Wafungwa 52 wafariki kabla ya kufikishwa mahakamani Madagascar

Wafungwa 52 wafariki kabla ya kufikishwa mahakamani Madagascar

Like
593
0
Tuesday, 23 October 2018
Global News

Shirika la kutetea haki za binaadamu, Amnesty International limesema watu 52 walikufa wakiwa kizuizini Madagascar mwaka uliopita kabla kesi zao hazijasikilizwa wakati nchi hiyo inakabiliwa na mfumo mbovu wa mahakama.

Hayo yameelezwa katika ripoti ya Amnesty International iliyotolewa leo ambayo imeonya kuwa asilimia 55 ya watu 11,000 waliofungwa magerezani nchini Madagascar walikuwa wakisubiri kesi zao zisikilizwe kwa mwaka uliopita wa 2017, licha ya wengi wao kukabiliwa na uhalifu wa makosa madogo, ambapo kwa mujibu wa sheria za kimataifa, bado hawana hatia.

Tamara Leger, mshauri na mtetezi wa haki za binaadamu wa Amnesty International nchini Madagascar, anasema kuwa utafiti wao unaonesha hali mbaya katika magereza ambako ni wazi watu wanakumbana na ukatili, vitendo visivyo vya kibinaadamu au vya kudhalilisha na wengine wanakabiliwa na utapiamlo mbaya.

Uhaba wa chakula

”Tumegundua kuwepo kwa uhaba wa chakula, ukosefu wa huduma za afya, wafungwa kukataliwa kuonana na ndugu zao na kati ya asilimia 80 na 90 ya watuhumiwa hawajaonana na mawakili wao. Mazingira haya yanakiuka sheria za kimataifa na kikanda, na hata sheria za Madagascar kwenyewe,” alisema Leger.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyopewa jina ”Kuadhibiwa Kutokana na Umaskini”, maafisa wa Amnesty International waliyatembelea magereza tisa ya Madagascar na watuhumiwa wengi wanashikiliwa kwa miaka mingi kwa sababu hawapelekwi kusikiliza kesi zao mahakamani. Kesi hizo huwa zinasomwa mara mbili tu kwa mwaka.

Mkurugenzi wa shirika hilo kusini mwa Afrika, Deprose Muchena amesema kutokana na mfumo mbaya wa mahakama nchini Madagascar, watu wanateseka magerezani kwa miaka kadhaa kabla hawajapelekwa mahakamani.

Muchena anasema wengi wanaoshikiliwa kwa muda mrefu bila kufikishwa mahakamani wanatuhumiwa kwa makosa madogo. Ametolea mfano wa mwanaume mmoja anayeshikiliwa kwa miaka mitatu na nusu kwa kuiba ng’ombe.

Kauli ya rais

Rais wa muda wa Madagascar, Rivo Rakotovao ameiita ripoti hiyo ya Amnesty International yenye ”kusikitisha” na ”isiyokubalika”, akisema wakati mwingine majaji hawana njia mbadala zaidi ya kuwaweka watuhumiwa gerezani.

Aidha, Rakotovao amekiri kuwa magereza ya nchi hiyo hayana uwezo wa kuhifadhi idadi kubwa ya wafungwa na hayana ubora na kwamba hakuna mtu aliyefikiria kuwekeza katika magereza tangu nchi hiyo ipate uhuru wake, hali ambayo amesema inapaswa ibadilike.

Madagascar inategemea kwa kiasi kikubwa msaada wa kimataifa na watu wengi hawajafaidika na uchumi unaokuwa taratibu, ambapo asilimia 76 wanaishi katika umaskini uliokithiri.

 

cc;DW

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *