Serikali ya Nigeria imethibitisha kuwa wengi kati ya wanafunzi wa kike 110 waliokuwa wametekwa na kikundi cha Boko Haram zaidi ya mwezi mmoja uliopita wameachiwa Jumatano asubuhi.
Shirika la habari la AFP limeripoti kuwa wasichana hao waliletwa katika mji wa Dapchi ulioko upande wa Kaskazini mwa Nigeria wa Jimbo la Yobe baada ya wale waliokuwa wanawashikilia kuwarejesha katika msafara ulioandamana na magari 9.
Ripoti za vyombo vya habari zimesema wasichana watano kati ya hao walikufa wakati wakisafirishwa, lakini afisa wa serikali wa jimbo la Yobe amesema hili bado halijaweza kuthibitishwa.
Waziri wa Habari wa Nigeria Lai Mohammed amesema kuachiwa kwa wasichana hao mapema asubuhi “bila masharti” kulitokana na “juhudi za kisiri” zikisaidiwa na “baadhi ya marafiki wa nchi hiyo.”
“Wasichana 91 na mvulana mmoja wameelezewa kuwa wameachiwa. Hayo ndio yaliyojiri,” amewaabia waandishi.
“Wengi kati ya wasichana hao, wengi wa wanafunzi hao walioachiwa huru hawakuletwa wote sehemu moja. Waliachwa njiani na wao wenyewe walirudi majumbani kwa wazazi wao.
Vyanzo vya habari nchini Nigeria vimesema kuwa wakazi wa eneo la Dapchi walikuwa wanafurahia kuachiwa kwa watoto hao.
Wazazi ambao hapo awali walikuwa wanamsiba kwa kutekwa kwa vijana wao hivi sasa wanasheherekea kurudi kwao.