WATANZANIA wameshauriwa kutumia vyema elimu na ushauri unaotolewa na wataalam mbalimbali juu ya matumizi bora ya lishe ili kupunguza hali ya udumavu kwa watoto wanaozaliwa nchini.
Hayo yamesemwa leo bungeni mjini Dodoma na Naibu waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii mheshimiwa Kebwe Steven Kebwe wakati akijibu maswali kutoka kwa baadhi ya wabunge yaliyoelekezwa katika wizara hiyo kuhusu ushiriki wa serikali katika kupunguza tatizo la udumavu.
Mheshimiwa Kebwe amesema kuwa kwa kiasi kikubwa serikali inashiriki katika kuhakikisha kila mwananchi anapata uelewa juu ya suala hilo na kwamba kuna mikakati mingi ambayo imepangwa kutekelezwa ili kuwasaidia zaidi wananchi kuweza kupambana na utapia mlo.