Mahakama ya juu zaidi nchini Zimbabwe imetupilia mbali kesi iliyowasilishwa na upinzani ya kupinga kutolewa sarafu mpya ya noti sawa na sarafu ya dola ya marekani, wakati nchi hiyo inapokabiliwa na hali mbaya ya uchumi tangu iache kutumia sarafu yake mwaka 2009.
Mahakama ya katiba ilitoa uamuzi kuwa kesi iliyowasilishwa na kiongozi wa chama cha Zimbabwe People First ,Joice Mujuru ukiitaja kuwa uvumi.
“Mnadai kuwa noti hizo zitatolewa kinyume cha sheria lakini serikali imesema kuwa itafanya hivyo kuambatana na sheria, ni kwa misingi gani mnataka tuwaamini?” naibu jaji mkuu Luke Malaba, alinukuliwa na gazeti la serikali la Herald.
Noti za dola milioni 75 zikiwa katika noti za dola mbili na tano zitaanza kutolewa mwishoni mwa mwezi ujao.
Hatua hiyo inachukuliwa wakati Zimbabwe inakabiliwa na uhaba mkubwa wa sarafu ya dola, ambayo ni sarafu yake kuu tangu mwaka 2009.