Zuckerberg aomba radhi kwa sakata la Cambridge Analytica

Zuckerberg aomba radhi kwa sakata la Cambridge Analytica

Like
318
0
Thursday, 22 March 2018
Global News

Mark Zuckerberg

Zuckerberg aomba radhi kwa sakata la Cambridge Analytica
Mmiliki wa kampuni ya Facebook Mark Zuckerberg amevunja kimya cha siku tano tangu lilipofichuliwa sakata la kutumika data za watumiaji wa Facebook, kwa kusema kampuni yake ina wajibu wa kulinda data za watumiaji wake.

Zuckerberg amesema kuwa Facebook, ambao ni mtandao wa kijamii unaoongoza kwa kuwa na watumiaji wengi duniani, umechukua hatua kadhaa kuzilinda data hizo huku akikiri kuwa walifanya makosa na wanahitaji kuchukua hatua madhubuti kurekebisha makosa hayo.

Kauli yake inakuja kufuatia kadhia ya kampuni ya kutathmini taarifa na takwimu ya Cambridge Analytica kutumia taarifa binafsi za watumiaji takriban milioni 50 wa Facebook katika kuwashawishi kufanya maamuzi kwenye chaguzi zikiwemo za Marekani na Kenya.

Kampuni hiyo ya Cambridge Analytica inadaiwa kutumia data hizo kumsaidia Rais wa Marekani Donald Trump katika kampeini za kinyang’anyiro cha urais mnamo mwaka 2016 ambapo aliibuka mshindi. Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Zuckerberg amekiri kuwa kitendo hicho kilikuwa ukiukaji mkubwa wa uaminifu.

Sakata laisababishia Facebook hasara

Kufuatia sakata hilo, Facebook imepata hasara ya karibu dola bilioni 50 katika masoko ya hisa katika kipindi cha siku tatu zilizopita na tayari kesi zimeanza kufikishwa mahakamani na wanahisa waliopata hasara kutokana na mtandao huo wa kijamii kuwapotosha kuwa una uwezo wa kulinda data za watumiaji wake.

Faceboook imesema inapanga kufanya uchunguzi wa kina dhidi ya maelfu ya App ambazo zinashirikisha Facebook, kuzuia wabunifu wa APP hizo fursa ya kupata data na kuwapa watumiaji wa facebook uwezo wa kuzuia data zao kupatikana kwa urahisi.

Hata hivyo mipango hiyo haijumuishi kupunguzwa kwa uwezo wa wafanyabiashara wanaotangaza biashara zao kupitia facebook kupata data. Matangazo ya kibiashara ndiyo uti wa mgongo wa kampuni hiyo kujipatia faida.

Bunge la Marekani na la Umoja wa Ulaya yamemtaka Zuckerberg kufika mbele yao na kutoa maelezo kuhusu sakata hilo. Mfichuzi wa sakata la Cambridge Analytica Christopher Wylie amesema amekubali mialiko ya kutoa ushahidi mbele ya wabunge wa Marekani na Uingereza.

Serikali ya Ujerumani imesema Facebook sharti iipe maelezo iwapo data binafsi za watumiaji milioni 30 wa Facebook nchini humo zimelindwa dhidi ya matumizi mabaya. Zuckerberg amesema Facebook imejitolea kuzuia uingiliaji wa chaguzi ndogo Marekani zitakazofanyika mwezi Novemba, uchaguzi mkuu wa India na Brazil.

Siku ya Jumanne bodi ya Cambridge Analytica ilimsimamisha kazi mkurugenzi mkuu mtendaji Alexander Nix ambaye alirekodiwa kwa siri akijigamba jinsi walivyochangia pakubwa kumpa Trump ushindi.

 

Comments are closed.