RAIS wa Ufaransa Francois Hollande na Meya wa mji wa Paris Anne Hidalgo waliweka bango la taarifa katika eneo la Place de la Republique kuwakumbuka watu 147 waliouawa katika mashambulizi ya kigaidi katika mji mkuu wa Ufaransa, Paris mnamo mwezi Novemba mwaka jana.
Rais Hollande aliungana na viongozi wengine na maelfu ya raia kuwakumbuka wahanga hao wa mashambulizi ya kigaidi ambayo kundi la wanamgambo wenye itikadi kali wa Dola la Kiislamu IS lilidai kuhusika.
Wiki nzima iliyopita, Ufaransa imekuwa ikiendesha shughuli za kuwakumbuka wahanga wa mashambulizi mbali mbali ya kigaidi ikiwemo shambulizi dhidi ya gazeti la tashtit la Charlie Hebdo.