WAZIRI wa mambo ya nje wa Ubelgiji Didier Reynders amesema mshukiwa mkuu wa mashambulizi ya kigaidi ya Paris, Salah Abdeslam, alikuwa anapanga kufanya mashambulizi katika mji mkuu wa Ubelgiji, Brussels.
Reynders amesema wamepata silaha nyingi, nzito na katika chunguzi za awali tangu kukamatwa kwa mshukiwa huyo, wamegundua mtandao mpya mjini Brussels unaohusishwa naye.
Abdeslam anazuiwa katika gereza lenye ulinzi mkali huku akiwa amefunguliwa mashitaka ya mauaji ya kigaidi kwa kuhusika katika mashambulizi ya Novemba 13 mwaka jana mjini Paris nchini Ufaransa yaliyosababisha vifo vya watu 130.