Erdogan: Tunasubiri matokeo ya uchunguzi kuhusu Khashoggi

Erdogan: Tunasubiri matokeo ya uchunguzi kuhusu Khashoggi

Like
505
0
Tuesday, 09 October 2018
Global News

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema atasubiri matokeo ya uchunguzi kuhusu kutoweka kwa mwandishi wa habari Khashoggi kabla kufanya maamuzi. Polisi wanaamini Khashoggi aliuawa na maafisa waliotumwa Istanbul

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema kuwa anasubiri matokeo ya uchunguzi kuhusu kutoweka kwa mwandishi habari wa Saudi Arabia Jamal Khashoggi, ambaye chanzo cha habari serikalini kilisema aliuawa ndani ya ubalozi mdogo wa Saudi Arabia ulioko Istanbul.

Jamal Khashoggi mwenye umri wa miaka 59 na ambaye ni mwandishi wa habari wa gezeti la Washington Post, alitoweka baada ya miadi na maafisa wa Saudi Arabia siku ya Jumanne.

Khashoggi alienda katika ubalozi huo kutafuta vyeti vinavyohitajika kumwezesha kumuoa mchumba wake.

Chanzo cha habari katika serikali ya Uturuki kililiambia shirika la habari la AFP kuwa polisi wanaamini Khashoggi aliuawa ndani ya ubalozi wa Saudi Arabia mjini Istanbul, madai ambayo Saudi Arabia imeyakanusha vikali.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema atasubiri matokeo ya uchunguzi kabla kufanya maamuzi.

Waandamanaji wakibeba picha za mwandishi habari Jamal Khashoggi wakati wa maandamano nje ya ubalozi wa Saudi Arabia mjini Istanbul.

“Kwa sasa tunasubiri kuona kile mwendesha mashtaka ataamua, kile atakachotangaza kutokana na matokeo ya uchunguzi. Kwa sababu, inasikitisha sana kwetu kwamba hili limetokea katika taifa letu. ” Amesema Rais Erdogan.

Uchunguzi za picha za ubalozi na uwanja wa ndege

Rais Erdogan amesema polisi wanachunguza picha za kamera za usalama CCTV katika milango ya kuingia na kutoka ubalozi huo na ya uwanja wa ndege wa Istanbul.

Gazeti la Washington Post, limesema Marekani inapaswa kutafuta majibu kutoka kwa Saudi Arabia kuhusu kutoweka kwa mwandishi wao wa habari, na kuichukulia hatua ikiwa ushirikiano utakosekana.

Canada pia imeelezea wasiwasi kuhusu ripoti kwamba Jamal Khashoggi aliuawa katika ubalozi wa nchi yake mjini Istanbul, Uturuki.

Hapo awali, polisi ya Uturuki ilisema, takriban Wasaudi Arabia 15, wakiwemo maafisa waliwasili kwa ndege mbili siku ya Jumanne na walikuwa ubalozini wakati sawa na Khashoggi.

Jamal Khashoggi amekuwa mkosoaji wa sera za mwana mfalme Mohammed bin Salman ambaye ni mrithi wa ufalme.

Duru ya pili serikalini imeliambia shirika la AFP kuwa kutokana na matokeo ya awali ya uchunguzi, polisi wanaamini Khashoggi aliuawa na maafisa waliotumwa Istanbul na walioondoka siku hiyo hiyo.

Polisi imenukuliwa na shirika la habari linalomilikiwa na serikali ya Uturuki, Anadolu ikisema kuwa mwandishi huyo wa habari aliingia ubalozini lakini hakutoka.

Kupitia ukurasa wa mtandao wa Twitter, ubalozi wa Saudi Arabia mjini Istanbul, umekanusha madai kwamba Khashogi aliuawa humo ndani ukisema ni madai yasiyokuwa na msingi.

Khashoggi amekuwa mkosoaji wa baadhi ya sera za mwana mfalme Mohammed bin Salman ambaye ni mrithi wa kiti cha ufalme, pamoja na na juhudi za Saudi Arabia katika vita nchini Yemen.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *