Rais wa Rwanda Paul Kagame amefanya mabadiliko makubwa katika baraza lake la mawaziri na kumteua Dkt Richard Sezibera kuwa waziri mpya wa mashauri ya nchi za nje.
Jenerali James Kabarebe aliyekuwa mtu wa karibu sana na Rais Kagame amepoteza wadhifa wake kama waziri wa ulinzi na badala yake akateuliwa mshauri wa rais katika masuala ya usalama.
Katika mabadiliko makubwa na ya kushtukiza aliyofanya Rais Kagame wizara 8 kati ya 23 zimepata mawaziri wapya zikiwemo wizara nyeti tatu, wizara ya ulinzi ambayo sasa inaongozwa na Meja jenerali Albert Murasira aliyechukua nafasi ya Jenerali James Kabarebe.
Katika mabadiliko makubwa na ya kushtukiza aliyofanya Rais Kagame wizara 8 kati ya 23 zimepata mawaziri wapya zikiwemo wizara nyeti tatu, wizara ya ulinzi ambayo sasa inaongozwa na Meja jenerali Albert Murasira aliyechukua nafasi ya Jenerali James Kabarebe.
Jenerali Kabarebe ndiye mtu aliyewahi kuwa mkuu wa majeshi ya nchi mbili Rwanda na Congo wakati wa utawala wa hayati Laurent Desire Kabila; kabla ya kuwa waziri wa ulinzi wa Rwanda kuanzia mwaka 2010.
Mwanajeshi huyo ni miongoni mwa maafisa saba wakuu wa Rais Kagame ambao walikuwa wamefunguliwa mashtaka na Ufaransa kuhusiana na kuuawa kwa aliyekuwa rais Juvenal Habyarimana, mauaji ambayo yanadaiwa kuanzisha mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 ambapo watu zaidi ya 800,000 waliuawa, wengi wao Watutsi walio wachache.
Hakuna sababu iliyotolewa ya kuondolewa kwa Kabarebe kutoka kwenye wizara ya ulinzi lakini kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, kuondoka kwake kunaonekana kama hatua kubwa katika kutaka kurejesha tena uhusiano mwema kati ya rwanda na Uganda.
Uhusiano wa Rwanda na jirani yake Uganda umekuwa ukidorora kwa miaka mingi, ambapo Rwanda imekuwa ikiituhumu Uganda kwa kuwakamata kiholela raia wake nchini humo na pia kwa kutoa hifadhi kwa waasi na wapinzani.
Uganda nayo imekuwa ikiituhumu Rwanda kwa kufanya ujasusi na kuingilia idara zake za usalama.
Mwezi Juni, uhusiano ulipokuwa umedorora zaidi, Jenerali Kabarebe aliituhumu Rwanda kwa kuwakamata kiholela na kuwatesa raia wa Rwanda.
Amekuwa akisema wazi kwamba Uganda inaionea kijicho Rwanda kutokana na maendeleo ambayo yamefkiwa na kuwatahadharisha raia wa Rwanda dhidi ya kwenda kutafuta kazi Uganda.
Aliyechukua mikoba yake ni Meja Jenerali Albert Murasira anayefahamika kuwa miongoni mwa maafisa waliokuwa katika jeshi la hayati Juvenal Habyarimana kabla ya kuunganishwa na jeshi la RPF na kufanya jeshi la taifa, RDF.
Wizara nyingine ni wizara ya mashauri ya nchi za nje ambayo sasa inaongozwa na balozi Dkt Richard Sezibera.
Si mgeni katika siasa za Rwanda na kimataifa, mbali na nyadhifa za uwaziri hapa Rwanda, Sezibera alishika wadhifa wa katibu mkuu wa jumuiya ya afrika mashariki.
Amechukua nafasi ya Louise Mushikiwabo ambaye aliteuliwa kuwa katibu mkuu wa jumuia ya nchi zinazozungumza lugha ya Kifaransa.
Kadhalika wizara ya mambo ya ndani ina waziri mpya ambaye ni Professa Anastase Shyaka aliyekuwa mkuu wa mamlaka ya utawala bora, amechukua nafasi ya Francis Kaboneka hii ikiwa ni baada ya msururu wa matukio ya wakuu wa wilaya kadhaa na wasaidizi wao kujiuzulu, baadhi kwa kashfa za ufisadi na wengine kushtumiwa kutokuwa karibu na wananchi.
Mabadiliko yaliyofanywa na Rais Kagame yanayoonekana kuwa ya kuleta damu mpya katika utawala wake, yamegusa pia baadhi ya taasisi nyingine.
Katika idara za usalama, aliyekuwa kamishna mkuu wa polisi IGP Emmanuel Gasana amepoteza nafasi yake iliyochukuliwa na aliyekuwa naibu wake Dan Munyuza, mkuu wa zamani wa idara ya upelelezi.