Bobi Wine aendelea kuitikisa Uganda

Bobi Wine aendelea kuitikisa Uganda

Like
625
0
Thursday, 27 December 2018
Global News

Nyota wa muziki wa pop na mbunge wa upinzani nchini Uganda Bobi Wine ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi Ssentamu amekataliwa kufanya tamasha lake leo Disemba 26 kama alivyokuwa amepanga hapo awali.

Msemaji wa polisi nchini Uganda, Emilian Kayima amesema kwamba Bobi Wine alikuwa hajaandika barua ya kuomba ruhusa kufanya tamasha hilo ndio maana hawawezi kumruhusu.

“Tutakuwa katika ufukwe wa Busabala kuzuia shughuli hiyo na kuhakikisha usalama upo.Tamasha hili halikuwa limeruhusiwa kufanyika kwa sababu ya kutokidhi vigezo”, Kayimba alisema.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Monitor la nchini Uganda limeeleza kwamba mapema leo, Bobi Wine aliandika kwenye mtandao wa kijamii kuwa kikosi cha usalama kimevamia tamasha lake la ‘One Love Beach in Busabala’na kuwakamata wafanyakazi wake.

Hili lingekuwa tamasha la pili la Bobi Wine kufanyika, tangu ashtakiwe na kufungwa kwa mshtaka ya uhaini.

Mwanzoni mwa mwezi Novemba mwanamziki huyo aliruhusiwa kufanya tamasha lake la kwanza kwa sababu lilikuwa la kiburudani na halikuwa la kisiasa.

Maelfu ya watu waliohudhuria tamasha hilo walivaa nguo nyekundu, rangi inayohusishwa na vuguvugu za Bobi Wine.

Lakini vilevile tamasha hilo lilikuwa na idadi kubwa ya polisi.

Bobi Wine anadaiwa kuteswa na kupigwa akiwa kuzuizi mwezi Agosti, madai yanayokanwa na mamlaka.

Bobi Wine na wenziwe 32 walikamatwa baada ya kudaiwa kushambulia msafara wa Rais wa Yoweri Museveni mjini Arua mwezi uliopita na kuwekwa katika kizuizi cha jeshi.

Watuhumiwa hao waliwekwa chini ya ulinzi wa jeshi huku Bobi Wine awali akipandishwa katika mahakama ya kijeshi kwa tuhuma za kumiliki silaha kinyume cha sheria.

Rais Yoweri Museveni alijitokeza na kukanusha taarifa kuwa Bobi Wine ameumizwa vibaya na kuvishutumu vyombo vya habari kwa kueneza taarifa za uongo.

Baada ya kelele za upinzani kupazwa ndani na nje ya Uganda pamoja na kwenye mitandao ya kijamii, kesi yake mbele ya mahakama ya kijeshi ilifutwa na kuachiwa huru kabla ya kukamatwa tena na kufunguliwa mashtaka ya uhaini katika mahakama ya kiraia.

Kabla hajakamatwa, Bobi Wine, alichapisha picha ya dereva wake ambaye alisema alipiwa risasi na kuuliwa na polisi waliodhani kuwa aliyekuwa ni yeye.

Bobi Wine alikamatwa tarehe 13 Agosti baada ya mkutano wa kampeni kaskazini-magharibi kwenye mji wa Arua ambapo kuna madai kuwa msafara wa rais ulitupiwa mawe.

Mwanamuziki huyo mwenye miaka 36 awali alishtakiwa kwenye mahakama ya kijeshi kwa makosa ya umiliki wa silaha kinyume cha sheria, mashtaka ambayo yalifutwa baadaye. Kisha akafunguliwa mashtaka ya uhaini kwenye mahakama ya kiraia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *