Shughuli za serikali ya Marekani kukwama msimu wa Krismasi

Shughuli za serikali ya Marekani kukwama msimu wa Krismasi

Like
423
0
Monday, 24 December 2018
Global News

Sehemu fulani ya shughuli za serikali ya Marekani zitaendelea kusitishwa kwa siku tano, baada ya wajumbe wa baraza la Seneti kushindwa kupiga hatua siku ya Jumamosi kutokana na mkwamo kwenye ufadhili wa ujenzi wa ukuta.

Kutokana na kusitishwa kwa shughuli za serikali, ambako kumeshuhudia baadhi ya mashirika yakisitisha operesheni zake siku ya Jumamosi (Disemba 22), Rais Donald Trump amesema atasalia mjini Washington katika sikukuu za Krismasi badala ya kwenda Florida.

Aliandika kupitia Twitter, “Niko Ikulu nikifanya kazi kwa juhudi. Tunaendelea kujadiliana na Democrats juu ya usalama wa mpaka unaohitajika (magenge, madawa ya kulevya, biashara haramu ya usafirishaji binadamu na mengine mengi), lakini tunaweza kutumia muda mrefu”.

Trump ameendelea kushinikiza juu ya mahitaji yake ya Dola bilioni 5 kuujenga ukuta katika mpaka wa Marekani na Mexico. Wademocrats wanapinga hilo, na kukosekana kwa mpango thabiti kunamaanisha fedha za shirikisho kwa ajili ya mashirika kadhaa zilikuwa zinaisha muda wake usiku wa Ijumaa.

Mabunge ya Baraza la wawakilishi na Seneti yalifanya vikao vyake siku ya Jumamosi, lakini pande zote ziliahirisha bila ya kufikia makubaliano, na hakuna kura iliyotarajiwa hadi Desemba 27.

Seneta wa Democrats Chuck Schumer

Seneta wa Democrat Chuck Schumer alimtuhumu rais Trump kwa kuchochea usitishaji wa shughuli za serikali: “rais Trump kama unataka shughuli za serikali kuendelea, achana na ukuta, ni hivyo rahisi tu na wazi”, alisema Schumer.

Shughuli muhimu za kiusalama za Marekani zimeendelea lakini wafanyakazi karibu 800,000 wa shirikisho wameathirika wakati wengi wakichukua likizo bila ya malipo kabla ya sikukuu ya Krismasi na wengine wakifanya kazi bila ya malipo. Seneti tayari limeidhinisha sheria ya kuhakikisha kwamba wafanyakazi watalipwa hapo baadae, na baraza la wawakilishi nalo lilikuwa na uwezekano wa kufuata mkondo huo.

Wakati Wamarekani wengi na watalii wakianza msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka baadhi ya maeneo ya kupumzika yamefungwa kabisa, wakati mengine yakisalia wazi lakini bila ya huduma kwa wateja.

Hatua ya serikali kufunga shughuli zake katika kilele cha msimu wa sikukuu za Krismasi, ni ya tatu tangu Rais Donald Trump achukue madaraka chini ya miaka miwili iliyopita.

Hatua hiyo imekuja wakati mgumu katika Ikulu ya White House, baada ya mkuu wa utumishi, John Kelly, na waziri wa ulinzi, Jim Mattis, kujiuzulu.

Trump alichochea hatua hiyo ya kufungwa kwa shughuli za serikali wakati alipokataa kusaini mswada wa bajeti ya muda mfupi kwa sababu haikujumuisha dola bilioni 5.7 anazohitaji kwa ajili ya ujenzi wa ukuta.

Bunge la Seneti liliendelea na vikao vyake Jumamosi mchana lakini wabunge wanasema hakuna hatua iliyopigwa, na masaa machache baadaye bunge liliahirishwa.

Nancy Pelosi akizungumza na waandishi wa habari

Afisa mmoja wa ngazi ya juu amesisitiza kwamba rais yuko tayari kukutana na mahasimu wake kutoka Democrats lakini ufadhili wa ukuta ni lazima. “Matumaini yetu ni kwamba sehemu fulani ya usitishaji shughuli za serikali kutasalia kwa siku chache. Kunaweza kusalia kwa muda mrefu, lakini hilo silo tunalotumaini”, alisema afisa huyo.

Wakati huo huo soko la hisa la Marekani limekabiliwa na wiki mbaya tangu mgogoro wa kifedha wa 2008. Wasiwasi juu ya kufungwa kwa shughuli za serikali kumechangia hali hiyo.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *