Tshisekedi na Kabila watangaza serikali ya Muungano

Tshisekedi na Kabila watangaza serikali ya Muungano

Like
875
0
Thursday, 07 March 2019
Global News

Kiongozi mpya katika Jamhuri ya Kidmeokrasi ya Congo, Felix Tshisekedi na mtangulizi wake Joseph Kabila wamesema wameamua kuunda serikali ya muungano kufuatia mazungumzo, shirika la habari la AFP linaripoti.

Licha ya ushindi wa rais Tshisekedi — kiongozi huyo amejikuta akilazimika kugawanya uongozi tangu uchaguzi huo wa urais.

Mpaka sasa hajafanikiwa kumteua waziri mkuu kutokana na kwamba muungano wa Kabila – Common Front for Congo (FCC) una uwingi katika bunge la taifa.

Mkwamo huo umeweka kizuizi kwa maazimio ya Tshisekedi kuigeuza nchi hiyo inayogubikwa kwa rushwa na tuhuma za ukiukaji wa haki za binaadamu.

Katika taarifa ya pamoja hapo jana Jumatano, Tshisekedi na Kabila wamesema kwamba licha ya “FCC kuwa na uwingi mkubwa bungeni” katika kuidhinisha matakwa yalioelezewa na wapiga kura, FCC na CACH wanaonesha uwajibikaji “wa malengo yao ya pamoja kuongoza pamoja kama sehemu ya serikali ya muungano” linaripoti AFP.

Taarifa hiyo inafuata ziara ya Tshisekedi nchini Namibia wiki iliyopita ambapo alielezea kukasirishwa kwake kwa kutoweza kuwa na uwingi kuunga mkono chaguo lake la wadhifa wa waziri mkuu.

Kwa miaka 18 iliyopita, taifa lenye utajiri wa madini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo limeongozwa na mtu mmoja: Joseph Kabila.

Kwa muda ilionekana kana kwamba Tshishekedi, jina lake halingekuwa kwenye karatasi za kura.

Kuongezea hilo, wakosoaji wake pia walikuwa wakisema Tshisekedi hajawahi kushikilia wadhifa wowote wa juu au kuwa na uzoefu wa usimamizi.

Lakini kadri muda ulivyosogea amefanikiwa kupanda cheo, kuanzia mwaka 2008 ambapo alikuwa katibu wa taifa aliyeangazia masuala ya uhusiano wa nje.

Tshisekedi, ingawa hana uungwaji mkono mkubwa kama wa babake, mwaka jana alisema kwamba akishinda urais ataunda tume ya ukweli, haki na maridhiano na kumuwajibisha Bw Kabila. Lakini alisema atamruhusu kusalia nchini DR Congo.

Changamoto kubwa ni kuangalia vipi Tchisekedi anaweza kuleta amani na maridhiano kwa taifa hilo hususan eneo la mashariki ambako kumeshuhudia ghasia na umwagikaji damu mkubwa wa raia, na uwepo wa wanamgambo waliojihami wanaotekeleza mashambulio.

Ni wazi kwamba ni wakati wa kihistoria kwa upinzani wa nchi hiyo, ambao umekuwa kando kando katika siasa za nchi kwa miongo kadhaa.

Lakini swali kubwa sasa ni je makubaliano haya ya kuunda serikali ya muungano yana uzito kiasi gani katika ushawishi wa kiongozi huyu mkuu, na inaweka wapi matumaini ya raia wa Congo katika swala la mageuzi nchini?

cc;BBCswahili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *