Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako ameagiza vyuo vyote nchini kuhakikisha hadi kufikia ijumaa Juni 5, mwaka huu viwe vimeshawalipa wanafunzi wote fedha zao za kujikimu na ambao hawatafanya hivyo watachukuliwa hatua.
Waziri Ndalichako ametoa agizo hilo leo Juni 3, jijini Dar es Salaam wakati akikabidhi magari manne kwa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) ambacho ni miongoni mwa vyuo vinne vitakavyonufaika na mkopo wa Benki ya Dunia kupitia mradi wao wa Kuleta Mapinduzi kwenye elimu ya ufundi Afrika Mashariki (EASTRIP).
Profesa Ndalichako amesema kuna baadhi ya vyuo mpaka leo bado havijawapatia wanafunzi fedha hizo za kujikimu licha ya kwamba Serikali imeshazitoa hivyo anatoa siku tatu kuanzia leo kuhakikisha wanazitoa ili wanafunzi waendelee na masomo bila kupata usumbufu wowote.