Afrika yaelekea kuzidiwa na watu

Afrika yaelekea kuzidiwa na watu

Like
631
0
Tuesday, 02 October 2018
Global News

Idadi ya watu barani Afrika inakuwa kwa kasi ambapo kufikia mwaka 2050 itakuwa imeongezeka maradufu ya ilivyo sasa, huku 40% ya watu masikini kabisa duniani wakihofiwa kuja kuishi kwenye mataifa mawili tu ya bara hilo.

Kwa sasa barani Afrika wanaishi watu bilioni 1.3. Miaka 32 ijayo, idadi hii itaongezeka mara mbili zaidi, na kama ukuwaji wa kiuchumi hautakwenda sambamba na ukuwaji huu wa idadi ya watu, basi kitakachotokea ni ongezeko la umasikini.

Khofu hiyo imeufanya Wakfu wa mwanzilishi wa kampuni ya Microsoft, Bill Gates, kufanya utafiti wa namna ya kukabiliana na kitisho kijacho. Yaliyogunduliwa na utafiti huo uliopewa jina “Walindamlango 2018” ni kwamba ikifika mwaka 2050, asilimia 40 ya watu walio masikini sana duniani watakuwa wanaishi kwenye mataifa mawili tu: Nigeria na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Hivi sasa, Nigeria inakaliwa na watu milioni 190, ambapo kwa wastani mwanamke mmoja huzaa watoto watano, na hilo lina matokeo yake, kwa mujibu wa Farouk Jega, mkurugenzi wa Wakfu wa Bill na Melinda Gates nchini Nigeria:

“Tayari hali ni mbaya hapa Nigeria. Umasikini wa kutupwa unazalisha hali ya ukosefu wa usalama, machafuko, uhalifu. Lakini serikali ya Nigeria inajaribu kukabiliana na ongezeko hili la kupindukia la idadi ya watu. Waziri wa afya anapigia kampeni njia za kisasa za uzazi wa mpango. Lakini ni asilimia 10 ya wanawake wanaotumia njia hizo, ambayo ni idadi ndogo. Gharama pia ni kubwa, hasa kwa wanawake na familia za kimasikini,” anasema Jega.

Kama ilivyo kwenye mataifa mengine mengi ya Afrika, jukumu la mwanamke nchini Nigeria ni lile lile la kuzaa, kulea watoto na kuhudumia nyumba. Serikali ya Nigeria inapambana kubadili mtazamo huu kwa kushirikiana na asasi za kijamii, viongozi wa kidini na kimila, anasema Faouk Jega, ambaye anaona kuwa kuna aina fulani ya mafanikio kwenye ushirikiano huu.

Angalau sasa raia wako tayari kujadili faida na hasara za kuwa na watoto wengi na ile mila kwamba mwenye watoto wengi anakuwa amejijengea uhakika wa kuwa na watu wa kumuangalia afikiapo umri wa uzee. Hata hivyo, naye mkurugenzi huyo wa Wakfu wa Bill na Melinda Gates nchini Nigeria, anakiri kuwa: “Panahitajika juhudi kubwa zaidi kubadili imani na mitazamo ya watu.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *