MAHAKAMA kuu ya Tanzania kitengo cha Ardhi leo inatarajia kutoa maamuzi juu ya ombi la dharura la kutaka zoezi la bomoabomoa kusitishwa katika kipindi ambacho kesi hiyo ipo Mahakamani.
Wakili wa mshitaki Abubakari Salim amesema kutokana na uwepo wa kesi mahakamani juu ya wananchi kutotendewa haki katika zoezi la kubomoa nyumba za mabondeni iliyofunguliwa na Mbunge wa Jimbo la Kinondoni Maulidi Mtulia waliamua kupeleka hati ya dharura ya kutaka zoezi hilo kusitishwa wakati kesi hiyo ikiendelea mahakamani.
Jaji wa Mahakama hiyo Panteline Kente amepokea ombi hilo la zuio na kuahidi kulitolea maamuzi leo ambapo amebainisha kuwa upande wa Serikali umepewa muda wa siku saba kutoa maelezo yao kuhusiana na uhalali wa zoezi hilo pamoja na kujibu madai yaliopo katika kesi.