Mfanyakazi mmoja nchini Australia amefungua mashtaka kwenye mahakama ya rufaa ya nchi hiyo akidai bosi wake alikuwa akimbughudhi ofisini kwa kujamba sana.
Awali, mahakama moja ya chini ilifikia uamuzi kuwa hakukuwa na bughudha yeyote katika suala hilo.
Hata hivyo, David Hingst anadai kuwa bosi wake wa zamani Greg Short alikuwa “akinyanyuka na kumjambia” karibu mara sita kwa siku.
Mwaka jana mashtaka dhidi ya kampuni yake ya zamani na kudai dola milioni 1.28 yalitupiliwa mbali na Mahakama Kuu ya Victoria iliyohukumu kuwa hakukuwa na bughudha.
Bwana Hingst mwenye miaka 56, amedai kuwa mashuzi hayo yamemsababishia “msongo mkubwa”.
‘Aalikuwa akijamba na kwenda zake‘
Hingst, ambaye alikuwa afisa utawala katika mji wa Melbourne, ameishtaki kampuni ya Construction Engineering mwaka 2017 lakini kesi hiyo ilitupwa Aprili 2018.
Amekata rufaa dhidi ya uamuzi huo na Jumatatu, Novemba 25 alisikilizwa na Mahakama ya Rufaa.
“Nilikuwa nikikaa kwenye chumba kidogo ambacho hakina madirisha, alikuwa akiingia na kujamba nyuma yangu na kisha kwenda zake. Alikuwa akifanya hivyo mara tano mpaka sita kwa siku,” Hingst ameliambia Shirika la Habari la nchi hiyo, Australian Associated Press (APP).
Katika kesi ya awali mwaka jana, bwana Short alidai kuwa hakumbuki kujamba akiwa karibu na Hingst lakini “yawezekana ilitokea mara moja ama mbili hivi, yawezekana.”
Hata hivyo, alikanusha kuwa alifanya vitendo hivyo “kwa madhumuni ya kumkera na kumbughudhi” Hingst.
Hingst alikuwa akimuita Short “Bwana Mnukaji” na alikuwa akipuliza uturi kila aliposogea karibu yake, korti iliambiwa.
Kwa mujibu wa mitandao ya Australia, Hingst amedai kuwa, tabia ya Short ilikuwa ni sehemu ya mpango wa kumng’oa kazini na muda aliofanya kazi na Construction Engineering kulimsababishia majeraha ya kiakili. Pia amedai kuwa Short alikuwa akimkejeli kutokana na ufanisi wake na kumpachika jina la “bwege”.
Hingst amesema kesi yake ya kwanza haikuamuliwa kwa usawa, kudai jaji alimbagua.
Mahakama ya Rufaa itatoa hukumu yake Ijumaa, Machi 29.