Dar es Salaam; Salama zaidi kwa wanawake afrika mashariki

Dar es Salaam; Salama zaidi kwa wanawake afrika mashariki

Like
719
0
Tuesday, 02 October 2018
Local News


Jiji la Dar es Salaam nchini Tanzania ndilo jiji ambalo wasichana na wanawake wanajihisi wakiwa salama zaidi miongoni mwa miji mikuu ya kibiashara Afrika Mashariki.

Hii ni kwa mujibu wa ripoti kuhusu usalama wa wanawake na wasichana dhidi ya udhalilishaji katika miji mbalimbali duniani uliofanywa na shirika la Plan International.
Jiji la Kampala linaongoza kwa kuwa hatari zaidi, ambapo wataalamu wanasema wasichana na vijana wa kike wamo katika hatari ya juu zaidi ya kudhalilishwa wa kingono wakiwa katika maeneo ya umma.
Sharon, mama mwenye miaka 19 anayeishi mtaa wa mabanda Kampala, aliambia Plan International kwamba matokeo hayo si ya kushangaza hata kidogo.

Utafiti huo uliangazia miji 22 na kuwahusisha wataalamu wa masuala ya haki za watoto na wanawake karibu 400 katika miji hiyo.
Wataalamu walikadiria hatari kwa kueleza miji waliyohisi ina hatari ya juu na hatari ya juu zaidi.

Katika miji ya Bogota na Johannesburg, kulikuwa na maafikiano kwamba si salama hata kidogo.
Kwa jumla, mji wa tatu duniani kwa kutokuwa salama kwa wanawake ni Delhi kisha inafuata Lima kabla ya kufikia Kampala.
Mji wa Kampala hata hivyo unaongoza kwa kuwa na kiwango cha juu cha ‘hatari kuwa juu zaidi’.

Jiji kuu la Kenya, Nairobi linaifuata Kampala ingawa kwa kiwango chake cha ‘hatari kuwa juu zaidi’ ni chini ya asilimia 40.
Baada ya Nairobi, kuna Cairo, Sao Paulo, Dhaka, Jakarta na Paris kabla ya kuifikia Dar es Salaam ambao ni mji wa 12 kwenye orodha ya jumla.

Kwa kuangazia unyanyasaji wa kingono na ubakaji, Johannesburg inaongoza ikifuatwa na Kampala, huku Nairobi ikiwa ya nne na Dar es Salaam ya 13.
Mmoja wa waliochangia kutoka Johannesburg alisema: “Unyanyasaji wa kingono hutokea mara nyingi sana kiasi kwamba tunahisi ni jambo tunalofaa kutafuta njia za kulizoea kuishi nalo na kuendelea na shughuli zetu.”
Kwa wizi na uchopozi, Johannesburg inaongoza, Kampala ni ya nne ikifuatwa na Nairobi. Dar es Salaam inapanda juu kidogo ikilinganishwa na visa vingine, ambapo hapa inashikilia nafasi ya 10.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *