Hatua ya Trump ya kuondoa majeshi ya Marekani yashangaza washirika wake

Hatua ya Trump ya kuondoa majeshi ya Marekani yashangaza washirika wake

Like
517
0
Thursday, 20 December 2018
Global News

Uamuzi wa Rais Donald Trump wa kuyaondoa majeshi ya Marekani kutoka nchini Syria umekosolewa vikali.

Bwana Trump alitoa tangazo hilo siku ya Jumatano, akisema kuwa kundi la Islamic State (IS) limeangamizwa.

Lakini washirika wake wakuu, wakiwemo viongozi wa chama chake cha kisiasa cha Republicans na mataifa ya kigeni, yamekanusha madai hayo, na kusema kwamba, hatua hiyo inaweza kufufua tena kundi la Islamic State (IS).

Vikosi vya Marekani vimesaidia pakubwa kuangamiza wanamgambo hao wa itikadi kali ya kijihad, kutoka maeneo ya Kaskazini Mashariki mwa Syria, lakini wapiganaji wachache wangali wakitekeleza uhasama wao katika maeneo hayo.

Seneta wa chama cha Republican Lindsey Graham, ambaye ni mmojawepo wa muugaji mkubwa wa Bw Trump, ameunga mkono uamuzi huo wa kujiondoa, akisema “ni sawa na kosa kubwa la Obama”.

Uingereza inatilia shaka hakikisho hilo la Trump iwapo kwa hakika kundi la IS limeangamizwa.

Pentagon inasema inajiandaa kwa “awamu nyingine ya kampeini kali” ya kuliangamiza kabisa kundi la IS, lakini haijatoa taarifa ya kina kuhusiana na hilo.

Rais Trump, ambaye kwa muda mrefu amekua akiahidi kuyaondoa majeshi ya Marekani kutoka Syria, ameandika katika mtandao wake wa Twitter kuwa, muda umewadia wa kuvirejesha vikosi vya kijeshi vya Marekani nyumbani baada ya “ushindi wao wa kihistoria”.

Seneta Graham, ambaye anaketi katika kamati maalum ya jeshi, ameonya kuwa, hatua hiyo ya kujiondoa itakuwa na “athari kubwa mno” ndani na nje ya Syria.

Amesema, kuna hofu kuwa, Urusi na Iran zitapata umaarufu mkubwa katika eneo hilo.

“Kujiondoa kwa Marekani wakati huu, kutakuwa ushindi mkubwa kwa ISIS [IS], Iran, Bashar al-Assad wa Syria, na Urusi,” amesema kwa njia ya taarifa.

Wakati huo huo, serikali ya Uingereza, imejitenga na maoni hayo ya Trump, kwamba kundi la IS limeshindwa.

“Mengi ingali kufanywa, na hatufai kupoteza muelekeo, wa hatari iliyopo,” taarifa kutoka kwa Wizara nchi za kigeni imesema.

Nayo Israel imesema kwamba, imeambiwa Marekani “ina mbinu nyingine ya kupata umaarufu katika maeneo hayo” lakini inafaa “kuchunguza muda na wakati [wa kujiondoa rasmi],namna itakavyofanywa na bila shaka athari ya hatua hiyo kwetu sisi”.

Huku akitumia tamko tofauti, msemaji wa Wizara ya mashauri ya nchi za kigeni wa Urusi Maria Zakharova, amesema kwamba uamuzi huo wa Marekani unaweza kuwa na matokeo “halisi ya namna ya kutanzua mzozo wa kisiasa” nchini Syria.

Serikali ya Uingereza inajihadhari tu- kutozungumza moja kwa moja mbele ya umma – au kulaani hatua ya Rais Trump, ya kuondoa majeshi ya Marekani kutoka Syria.

Inasemekana kuwa, kundi la wapiganaji wa IS lingali likitoa tishio kubwa licha ya “makabiliano makali dhidi yake” ambayo yametekelezwa hivi majuzi.

Nchini Syria, majeshi ya Wakurdi ambayo inapambana na IS, inajihisi kutengwa, sawa tu na namna Uturuki, inavyoapa kuzidisha mashambulio yake dhidi ya Wakurdi. Washirika wakuu zaidi wa utawala wa rais wa Syria, Bashar al-Assad, Urusi na Iran, wamefurahia sana uamuzi huo wa Trump.

Wanadhani hiyo sasa ina maana ya kuongeza nguvu zao maradufu ndani na je ya Syria.

Zaidi ya wanajeshi 2,000 wa Marekani, wamo maeneo ya Kurdish, Kaskazini mwa Syria.

Ushirikiano wa majeshi ya muungano ya Syrian Kurdish na wapiganaji wa Kiarabu, maarufu kwa jina Syrian Democratic Forces, unasifiwa kwa kuhusika katika kuliangamiza kundi la IS, baada ya kusambaratisha kabisa ngome zake nchini Syria, miaka minne iliyopita.

Licha ya hayo yote, wanamgambo hao bado hawajaangamizwa kabisa

Ripoti ya hivi punde ya Marekani, inasema kwamba, kuna wanamgambo wapatao 14,000 wa IS nchini Syria na hata zaidi katika taifa jirani la Iraq – huku kukiwa na hofu, kuwa wataamua kutumia mbinu za kuvizia na kushambulia maarufu kama vita vya Kigorilla katika harakati za kuimarisha tena mtandao wao.

Lakini ushirikiano kati ya Marekani na Wakurdi, yamehatarisha hali katika taifa jirani la Uturuki, ambayo inawaona wanamgambo wa Kikurdi wa YPG – kama wapiganaji wakuu wanaohatarisha jeshi la Syria- SDF – na kuwa kama kundi lililoharamishwa la wapiganaji wa Kikurdi, wanaotafuta kujitenga na kuwa na serikali yao mbali na utawala wa Uturuki.

Siku ya Jumatatu, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, alisema taifa lake, karibuni linajiandaa kuanzisha operesheni kali ya kijeshi dhidi ya kundi la YPG nchini Syria.

Bwana Erdogan, aidha aliongeza pia kuwa, amejadili mipango yake na Rais Trump kwa njia ya simu, na kwamba ameonyesha “kukubali”.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *