JONJO SHELVEY AITWA KIKOSINI UINGEREZA

JONJO SHELVEY AITWA KIKOSINI UINGEREZA

Like
211
0
Tuesday, 01 September 2015
Slider

Jonjo Shelvey ana kila sababu ya kuikumbuka siku ya Jumapili, kwani baada ya kusaidia Swansea City kulaza Manchester United 2-1 Ligi ya Premia, alitajwa kwenye kikosi cha Uingereza kitakachocheza mechi za kufuzu kwa Euro 2016 dhidi ya San Marino na Uswizi.

Kiungo huyo wa kati alichezea taifa mechi yake ya pekee dhidi ya San Marino miaka miwili iliyopita.

Beki wa kushoto wa Manchester United Luke Shaw, aliyechezea taifa mara ya mwisho ushindi wa 3-1 dhidi ya Scotland Novemba 2014, pia aliitwa tena kikosini.

Mchezaji pekee ambaye hajawahi kuchezea taifa hilo aliyetajwa kwenye kikosi hicho cha wachezaji 22 ni kipa wa Burnley Tom Heaton.

“Jonjo Shelvey amepata fursa nyingine kwani amekuwa akicheza vyema sana tangu mwanzo wa msimu,” kocha wa Uingereza Roy Hodgson alisema kwenye taarifa.

“Kikosi cha sasa hivi kinaonyesha tunatumia wachezaji kadha wazuri kwa lengo la kuwa na wachezaji wa kawaida kikosini Uingereza na kujitwalia tiketi Euro 2016.

“Kabla ya hapo kuna mechi mbili za kuangazia. Wachezaji lazima waendelee, kucheza vyema na kulenga kushinda kila mechi. Sitaki ulegevu wowote na tunataka kushinda mechi hizi mbili.”

Uingereza watakutana na San Marino ugenini Septemba 5 kabla ya kukabili Uswizi uwanjani Wembley siku tatu baadaye.

Wameshinda mechi zao zote sita za kufuzu kufikia sasa na wakizoa alama nne kutoka kwa mechi mbili zijazo basi watahakikishiwa kumaliza nambari wani au nambari mbili Kundi E na kufuzu kwa dimba hilo litakalochezewa Ufaransa mwaka ujao.

Wayne Rooney atafurahia sana kukabiliana na wanyonge San Marino. Mshambuliaji huyo wa Manchester United amefunga mabao 48 kimataifa na anahitaji bao moja zaidi kumfikia Bobby Charlton kuwa mfungaji mabao mengi zaidi timu ya taifa ya Uingereza.

Kikosi cha Uingereza

Magolikipa: Joe Hart (Manchester City), Jack Butland (Stoke City), Tom Heaton (Burnley).

Mabeki: Nathaniel Clyne (Liverpool), Luke Shaw (Manchester United), Kieran Gibbs (Arsenal), Gary Cahill (Chelsea), Chris Smalling (Manchester United), John Stones (Everton), Phil Jagielka (Everton).

Viungo wa kati: Michael Carrick (Manchester United), James Milner (Liverpool), Ross Barkley (Everton), Jonjo Shelvey (Swansea City), Ryan Mason (Tottenham Hotspur), Alex Oxlade-Chamberlain (Arsenal), Fabian Delph (Manchester City).

Washambuliaji: Raheem Sterling (Manchester City), Wayne Rooney (Manchester United), Harry Kane (Tottenham Hotspur), Jamie Vardy (Leicester City), Theo Walcott (Arsenal).

Comments are closed.