Kavanaugh akaribia kupitishwa jaji Mahakama ya Juu

Kavanaugh akaribia kupitishwa jaji Mahakama ya Juu

Like
436
0
Saturday, 06 October 2018
Global News

Kuna uwezekano mkubwa wa baraza la Seneti kumpitisha mteule wa Rais Donald Trump kwa nafasi ya jaji wa Mahakama ya Juu ya Marekani, Brett Kavanaugh, licha ya shutuma za mashambulizi ya ngono dhidi yake.

Katika hatua inayoonekana kama mafanikio makubwa kwa Rais Trump, wajumbe kadhaa wa Seneti walionesha uungaji mkono wao kwa uteuzi wa Jaji Kavanaugh, hata kutoka kundi la wabunge wa Democrat.

Seneta Susan Collins wa Republican na Joe Manchin wa Democrat walikuwa wa mwanzo kupiga kura za kumpitisha jaji huyo anayeandamwa na shutuma za kumdhalilisha kingono Profesa Christine Blasey Ford.

Matamshi ya wawili hawa yaliifanya idadi ya wajumbe waliokubali waziwazi kumuunga mkono jaji huyo mwenye umri wa miaka 53 kufikia 51 kati ya baraza lenye wajumbe 100, ingawa ithibati kamili isingeliweza kufahamika hadi jioni ya Jumamosi (Oktoba 6).

Collins, mbunge anayepigania haki ya kuchaguwa kutoka Maine, alisema Kavanaugh alikuwa na haki ya “kuchukuliwa kuwa hana makosa” kwani shutuma dhidi yake zilikosa ushahidi wa kumuhusisha na kosa analotuhumiwa nalo.

Licha ya kutambua kuwa ushahidi wa Profesa Ford ulikuwa wa kweli, wa uchungu na wenye nguvu na kwamba mlalamikaji ni mwathirika wa shambulizi la ngono, Collins aliongeza kwamba haamini kuwa shutuma hizo zinaweza kumzuwia Kavanaugh kuhudumu kwenye mahakama hiyo ya juu.

Muda mchache baada ya hotuba hiyo ya Collins, Manchin naye alitangaza kumuunga mkono, akimuita Kavanaugh kuwa ni jaji anayefaa zaidi na kwamba asingeliruhusu siasa za vyama kuathiri mwenendo wa mahakama.

Kinyume na Collins, Manchin anakabiliwa na shinikizo la hali ya juu, kwani anaingia kwenye uchaguzi katika jimbo lake la West Virginia, jimbo ambalo Trump alishinda kwa kishindo mwaka 2016.

Trump afurahia

Maandamano ya kupinga uteuzi wa Jaji Brett Kavanaugh nchini Marekani

Matokeo ya mwisho yalikuwa na mashaka, baada ya mjumbe mmoja wa Republican, Lisa Murkowski, kutangaza kukaidi msimamo wa chama chake na kupiga kura ya kumpinga Kavanaugh.

Trump aliandika kwenye mtandao wake wa Twitter kwamba alikuwa amefurahishwa sana na kura. “Ninajionea fahari kwa baraza la Seneti la Marekani kwa kupinga kura ya NDIO kuelekea kupitishwa kwa Jaji Brett Kavanaugh.”

Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Sarah Sanders, alimshukuru Collins kwa “kusimamia imani yako na kufanya kitu sahihi,” huku rais wa zamani, George HW Bush, akimpongeza kwa “ushujaa wake wa kisiasa na heshima.”

Uteuzi wa Kavanaugh ulikumbwa na msukosuko baada ya Profesa Ford kujitokeza mbele ya Seneti wiki iliyopita kuzungumzia shutuma za kubakwa na jaji huyo wakati wawili hao wakiwa wanafunzi wa sekondari ya juu miaka zaidi ya 30 iliyopita.

Ushahidi wake uliokuwa na taswira ya kutisha ulipelekea kucheleweshwa kwa kura ya kumuidhinisha Kavanaugh, huku ukiitishwa uchunguzi wa shirika la upelelezi la FBI. Hata hivyo, mawakili wa Profesa Ford wanasema uchunguzi huo haukutosha.

“Uchunguzi wa FBI ambao haujumuishi mahojiano na Dk. Ford na Jaji Kavanaugh hauna maana yoyote,” ilisema taarifa ya mawakili hao iliyosambazwa kwa vyombo vya habari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *