Kijana wa Kimaasai afunga ndoa na wanawake wawili wakati mmoja

Kijana wa Kimaasai afunga ndoa na wanawake wawili wakati mmoja

1
1368
0
Friday, 14 December 2018
Global News

Morani mmoja katika kaunti ya Kajiado nchini Kenya ameacha watu midomo wazi baada ya kufunga ndoa na wanawake wawili kwa mpigo.

Tom Mako, maarufu kama Junior, 27, alifanya sherehe hiyo ya harusi Jumanne wiki hii.

Mako anatokea kwenye familia ambayo ndo za wake wengi ama mitala ni jambo la kawaida.

Hata hivyo kuoa wake wawili kwa mpigo ni jambo ambalo halikuwahi kusikika katika jamii ya Kimaasai ambayo wanandoa hao wametokea. Wapo wanaume wanaowaoa wake wengi lakini si kwa wakati mmoja.

Katika harusi hiyo ambayo ilipambwa vilivyo katika kitongoji cha Kisaju, Mako aliwaoa Elizabeth Silamoi, 25, na Joyce Tikoyian, 23.

Wote wawili ni wanafunzi wa chuo kikuu cha Kenya Assemblies of God mjini Kitengela, si mbali sana na eneo Kisaju anakoishi Tom.

Huhudhuria masomo na kurejea nyumbani jioni. Wamekuwa pamoja kwa mwaka mmoja, na sherehe ya Jumanne ilikuwa ya kurasmisha ndoa kati ya kitamaduni.

Mako alikutana na Bi Silamoi miaka miwili iliyopita wakati akichunga ng’ombe zake karibu na nyumabni kwa mwananmke huyo.

Mwaka jana akakutana na Bi Tikoyian pia akiwa anachunga ng’ombe karibu na kwao.

Tikoyian amesoma mpaka kidato cha nne na Silamoi aliishia kidato cha tatu.

Katika mila za Kimasai, mahari ya ng’ombe hutolewa kabla ya kufungwa kwa ndoa, na bwana harusi Mako alikamilisha hilo ipasavyo.

Mako aliwaoa wakeze kimila japo wote walivalia mavazi ya kimagharibi. Mako alivalia suti ya rangi ya samawati na wakeze wakivaa mashela meupe. Wote pia walivalia urembo wa Kimaasai.

“Nataka kuliweka sawa hili, harusi yangu ilikuwa ya kimila na haikuwa na mahusiano yoyote na kanisa. Kuna watu wanatuma habari za kupotosha mitandaoni kuwa ndoa yangu ilisimamiwa na wachungaji,” Mako, ambaye ni mfanyabiashara, amenukuliwa na gazeti la kibinafsi la Star la nchini Kenya.

Amesema amewaoa wanawake hao kwa sababu wote wanampenda na hakutaka kumsononesha yeyote kati yao.

“Huu ni ujumbe ninaoutuma kwa waume wa kisasa wanaojifanya kuwa wanampenda mwanamke mmoja na huku wakiwalaghai kwa kuingia kwenye mahusiano na wengine pembeni,” amesema na kuongeza:”Nimekuwa muaminifu kwa wake zangu kwa sababu sitakuwa na sababu ya kuongeza mke mwengine. Ninaamini wawili watanitosheleza.”

Bi Silamoi ndiye aliyekuwa wa kwanza kuingia kwenye penzi na Mako, na kusema kabla ya kuja kwa mwenzake wawili hao walijadiliana kwa kina na kukubaliana.

“Ninampenda. Nilimpa Baraka zangu kuongeza mpenzi. Nampenda (mke mwenzake) pia.”

Bi Tikoyian, amesama wote wamekubaliana kuwa katika mahusiano ya aina hiyo na wazazi wake walikubali hilo kwa sababu wanamuamini Mako.

Wazazi wa bwana harusi,Bw Mako Busabus na Bi Sintiyio, wamesema hawakuamini mwanzoni mtoto wao alipowaambia anataka kuoa wake wawili kwa siku moja, na sherehe moja. Lakini hilo limepita

“Kwa umri wangu wa miaka 90 sijawahi kuona kitu kama hiki huku umasaini. Kwa kawaida, mtu anayetaka kuongeza mke husubiri kwanza walau baada ya mwaka au miaka miwili toka alipofunga ndoa ya kwanza,” amesema Busabus.

Mamorani wengine pamoja na wageni waliohudhuria harusi hiyo wanamchukulia Mkako kama shujaa kwa kufanya jambo ambalo halikuwahi kufanyika kabla umasaini.

Baada ya harusi, watatu hao wamekuwa wakiendelea na maisha yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *