Polisi mjini New York inachunguza vifo vya dada wawili kutoka Saudi Arabia ambao walipatikana wamefariki wakiwa wamefungwa pamoja katika mto Hudson wiki iliyopita.
Tala Farea, 16, na Rotana Farea, 22, walipatikana wakiwa wameelekeana uso kwa uso huku wakiwa wamevalia nguo zao na hapakua na ishara zozote za kuonyesha kuwa walipata usumbufu.
Wachunguzi wanasema ni mapema kubaini ikiwa uhalifu wowote ulifanyika au vifo vyao vilitokana na tukio la kujitoa uhai.
Polisi wanasema wasichana hao walikua wametoa maombi ya kutaka kupewa hifadhi nchini Marekani.
Kwa mujibu wa maafisa nchini Marekani dada hao wa Farea kutoka Saudi Arabia walihamia Fairfax, Virginia, mwaka 2015 wakiwa na mama yao, na walikua na tabia ya kutoroka nyumbani.
Wachunguzi wanasema bado ni ”kitendawili” jinsi walivyopatikana kwenye kingo za mto wakiwa wamefariki zaidi ya kilomita 400 kutoka nyumbani kawo.
Taarifa iliyotolewa na maafisa wa ubalozi wa Saudia inasema kuwa ubalozi huo uliwasiliana na familia yao na kuongeza kuwa dada hao walikua wanafunzi walikua ”wameandamana na kaka yao mjini Washington”.
Shirika la habari la Associated Press, linadai kuwa polisi ya New York, wanasema kuwa siku moja kabla ya miili yao kupatikana, mama yao alipokea simu kutoka ubalozi wa Saudia kuamuru familia yake kurejea nyumbani kwa sababu wasichana hao walikua wameomba kupewa hifadhi ya kisiasa.
Wasichana hao walipatikana katika ukingo wa bustani ya Riverside Jumatano iliyopita wakiwa wamevalia suruali nyeusi ya kubana na jaketi huku wakiwa wamefungwa pamoja katika sehemu za kiuno na miguu.
Awali polisi walisema wasichana hao huenda wamejirusha mtoni kutoka daraja la George Washington, lakini wakatilia shaka kauli hiyo baada ya kukosa majeruhi ya kawaida inayohusishwa na mtu aliyeanguka.
Baada ya kutoa michoro ya wasichana hao waliweza kutambua miili yao siku ya Ijumaa na sasa wanatoa wito kwa mtu yeyote aliye na ufahamu kuhusu maisha yao katika jiji la New York katika kipindi cha miezi miwili kuwasilisha taarifa hiyo kwao
Afisa mkuu wa upelelezi wa New York, Dermot Shea, amesema”Naamini uchunguzi ukikamilika tutabaini nini hasa kilichotokea.”
Cc;Bbcswahili