Kuna ‘mshindi wa wazi’ uchaguzi wa urais DRC

Kuna ‘mshindi wa wazi’ uchaguzi wa urais DRC

1
1380
0
Friday, 04 January 2019
Global News

Kanisa Katoliki, ambalo lina ushawishi mkubwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, limesema kuna mshindi wazi wa urais katika uchaguzi uliofanyika Jumapili, kwa mujibu wa matokeo ambao wamefanikiwa kuyaona.

Maaskofu wa kanisa hilo wamewataka watawala nchini humo kuwa wakweli na kutangaza matokeo hayo karibuni.

Kanisa hilo lina maelfu ya wangalizi wa uchaguzi nchini humo na baadhi wamewasilisha ripoti za dosari kadha wa kadha.

Tume ya uchaguzi ilitarajiwa kutangaza matokeo Jumapili lakini wiki hii ilidokeza kuwa huenda ikachelewa kufanya hivyo kwani bado haijapokea matokeo kutoka vituo vingi vya kupigia kura nchini humo.

Mkuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (CENI) Corneille Nangaa alisema matokeo ya zaidi ya asilimia 80 ya kura bado yanasubiriwa.

Upinzani pia umelalamikia dosari kwenye uchaguzi huo.

Rais Joseph Kabila anatarajiwa kuondoka madarakani baada ya kuongoza kwa miaka 17 na ameahidi kukabidhi madaraka kwa atakayeshinda uchaguzi.

Maafisa bado wanahesabu na kutathmini matokeo ya uchaguzi huo wa Jumapili

Baraza la Taifa la Maaskofu Congo (Cenco) halikusema nani linaamini alishinda uchaguzi huo.

Kanisa hilo limekuwa likipinga kuongezwa kwa muda wa Rais Kabila madarakani, tangu uchaguzi ulipoahirishwa mara kadha.

Bw Kabila awali alitarajiwa kuondoka madarakani 2016 lakini uchaguzi ukaahirishwa kutokana na kile serikali ilisema ni kutokamilika kwa maandalizi.

Mtandao na TV

Huku matokeo yakisubiriwa, serikali imefungia matangazo ya runinga inayomilikiwa na mwanasiasa wa upinzani.

Msemaji wa upinzani Lambert Mende aliituhumu Canal Congo kwa kutangaza matokeo ya uchaguzi kabla ya matangazo rasmi kutolewa.

Hatua hiyo imejiri siku chache baada ya huduma ya mtandao wa intaneti kuzimwa taifa lote.

Canal Congo inamilikiwa na mbabe wa kivita wa zamani Jean Pierre-Bemba.

Mashine za kielektroniki zilitumiwa katika shughuli ya kupiga kura kwa mara ya kwanza

Alizuiwa kuwania kutokana na kupatikana na hatia ya kuwahonga mashahidi katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) wakati wa kesi yake ya uhalifu wa kivita.

Anamuunga mkono mfanyabiashara Martin Fayulu.

Pamoja na kuifungia Canal Congo, seriali pia imefungia matangazo ya Radio France Internationale (RFI) na kufuta kibali cha mmoja wa waandishi wake, Florence Morice, wakimtuhumu kwa kuvunja sheria za uchaguzi.

Waangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika wameeleza uchaguzi huo wa Jumapili kama ulioendeshwa vyema.

Wagombea wa upinzani Martin Fayulu (kushoto) na Felix Tshisekedi (kulia) watakabiliana na Emmanuel Shadary (katikati ), aliyekuwa waziri wa maswala ya ndani.

Nani waliwania?

Kulikuwa na wagombea 21 lakini watatu ndio wakuu:

  • Emmanuel Ramazani Shadary, Waziri wa zamani wa mambo ya ndani na mtiifu kwa Kabila, ambaye aliwekewa vikwazo na Muungano wa Ulaya kwa hatua zilizochuliwa upinzani wakati wa maandamano ya mwaka 2017.
  • Martin Fayulu, Mkurugenzi mkuu wa zamani wa mafuta ambaye ameahidi nchi yenye mafanikio lakini ambaye watu maskini wanahisi hawezi kuwatetea.
  • Felix Tshisekedi Tshilombo, Mtoto wa mwanasiasa mkongwe ambaye ameahidi kupambana na umaskini.

cc;-BBCswahili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *