Leicester City watajizolea $200m (£150m) baada yao kufanikiwa kushinda Ligi Kuu ya Uingereza Jumatatu, watathmini wa michezo na utangazaji wa Repucom wanasema.
Pesa hizo zinatokana na tuzo ya kushinda Ligi ya Premia, pesa za kushiriki Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya, na ongezeko la mapato ya kila siku kutokana na mauzo ya tiketi.
Klabu hiyo pia itajivunia kupanda kwa thamani ya udhamini na pia ongezeko la mashabiki duniani.
Klabu hiyo inayotoka East Midlands itashiriki katika Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya msimu ujao jambo litakalowawezesha kutazamwa na watu wengi zaidi kwenye runinga Ulaya na kote duniani.
wachezaji wakisherehekea
Afisa mkuu wa ushauri wa kitaalamu wa Repucom Uingereza na Ireland Spencer Nolan anasema kwamba mashabiki huwa na umuhimu mkubwa kwa klabu na watachangia sana katika ukuaji wa Leicester kibiashara.
“Ingawa ni mapema sana kubaini ongezeko la mashabiki hasa bara Asia, mitandao ya kijamii inatupa fursa ya kufanya hili,” anasema.
Msimu huu, wafuasi wa Leicester City katika Facebook waliongezeka 540%, ongezeko kubwa zaidi miongoni mwa klabu za michezo duniani.
Nchini Algeria klabu hiyo ina wafuasi 500,000 kwenye Facebook, idadi kubwa zaidi katika nchi moja (16.7%), sana kutokana na mshindi wa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa PFA, winga Riyad Mahrez ambaye ni raia wa Algeria.
Kumeshuhudiwa pia ongezeko kubwa la mashabiki Thailand na Italia.
Mmiliki wa klabu hiyo Vichai Srivaddhanaprabha ni raia wa Thailand naye meneja Claudio Ranieri ni Mwitaliano.