Mapambano yapamba moto Hodeida

Mapambano yapamba moto Hodeida

Like
539
0
Wednesday, 07 November 2018
Global News

Wanajeshi wa serikali na waasi wamepambana tena leo karibu na mji wa bandari wa Yemen, Hodeida, ambao ni muhimu katika upitishaji wa msaada wa kiutu.

Siku tano za mapambano kati ya waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran na jeshi, likisaidiwa na muungano wa kikanda wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia, zimesababisha vifo vya Zaidi ya watu 150 katika mkoa wa Bahari ya Sham wa Hodeida.

Msemaji wa wa muungano unaoogozwa na Saudia amesema hawana mipango ya kufanya mashambulizi kamili ya kuukomboa Hodeida. Lakini maafisa kadhaa wa kijeshi kwenye eneo hilo wameripoti kuwa wanajeshi wao wameuzingira mji huo unaodhibitiwa na waasi.

Mapigano hayo yanakuja wakati Umoja wa Mataifa ukishinikiza kuanzishwa tena kwa mazungumzo kati ya pande zinazozana, baada ya mazungumzo kuvunjika jijini Geneva mwezi Septemba.

Hodeida ni mojawapo ya ngome za mwisho za Wahouthi katika mwambao wa magharibi mwa Yemen. Waasi hao waliikamata bandari hiyo pamoja na mji mkuu mnamo mwaka wa 2014.

Jeshi pinzani linaloongozwa na Saudia linaloishirikisha Umoja wa Falme za Kiarabu, limezikomboa bandari kadhaa za nchi hiyo.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwashughulikia Watoto – UNICEF ambalo linasema Yemen ni kama kuzimu, wiki hii umeonya kuwa shambulizi mjini Hodeida litazaathiri maisha ya watu wanaoishi mjini humo na kote nchini.

Mamilioni ya watu wanakabiliwa na njaa Yemen

Mashirika ya haki za binaadamu yanaonya kuwa Hodeida iko katika hatari kubwa ya kutokea janga kubwa. Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka – MSF limesema leo kuwa “wakati mapigano yakiongezeka Hodeida, MSF ina wahofia wagonjwa na wafanyakazi wa hospitali ya Al-Salakhana na maelfu ya wakaazi wanaoendelea kubakia mjini humo.

Mamilioni ya watu wanakabiliwa na njaa Yemen

Shirika la Save the Children limeripoti kuwa kulikuwa na karibu mashambulizi 100 ya kutokea angani mwishoni mwa wiki. Nalo Baraza la Wakimbizi la Norway limeonya kuwa mapigano na mashambulizi ya angani katika mkoa wa Hodeida yanaharibu Zaidi upatikanaji wa usalama na msaada kwa raia. Nchi hiyo maskini zaidi katika ulimwengu wa Kiarabu, Yemen sasa ni makao ya kile Umoja wa Mataifa unakiita kuwa mzozo mbaya Zaidi wa kibinadamu duniani. Takribani watu milioni 14 wanakabiliwa na kitisho cha njaa wakati vita vikiingia mwaka wake wa nne.

Serikali ya Yemen leo imeidhinisha bajeti mpya na hatua za kukusanya kodi zinazolenga kuipiga jeki Benki Kuu wakati mamilioni wakiendelea kukumbwa na kitisho cha njaa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *