Mshukiwa wa vifurushi vya mabomu akamatwa

Mshukiwa wa vifurushi vya mabomu akamatwa

Like
685
0
Saturday, 27 October 2018
Global News

 

Mtu anayeshukiwa kutuma kwa njia ya posta, vifurushi vya mabomu kwa wakosoaji wakubwa wa Rais Donald Trump wa Marekani amekamatwa jimboni Florida Ijumaa. Trump amesema ingawa mtu huyo ni mfuasi wake, hawezi kuwajibishwa.

Mtu huyo, Cesar Sayoc mwenye umri wa miaka 56, ana rekodi ya vitendo vya kihalifu, vikiwemo kutishia kuripua mabomu. Alikamatwa na maafisa wa usalama wa serikali kuu ya Marekani, nje ya kiwanda cha vipuri vya magari karibu na mji wa Miami. Helikopta zilikuwa zikizunguka juu ya eneo hilo alipotiwa mbaroni.

Maafisa hao wa usalama vile vile walilikamata basi dogo ambalo inaaminika ndilo maskani ya mshukiwa huyo. Vioo vya madirisha ya basi hilo vimefunikwa na karatasi zenye picha za Rais Trump, na maandishi ya kukikashifu kituo cha televisheni cha CNN. Karatasi nyingine zinaonyesha picha za viongozi wa chama cha Democratic, wakiwa wamewekewa vilengeo katika vichwa vyao.

Obama ni miongoni mwa walengwa

Cesar Sayoc, mshukiwa wa kutuma vifurushi vya mabomu Marekani

Miongoni mwa watu mashuhuri waliotumiwa vifurushi hivyo vya mabomu, ni aliyekuwa rais wa Marekani kabla ya Trump, Barack Obama, na Hillary Clinton ambaye alipambana na Trump katika uchaguzi wa rais uliopita.

Alama za vidole pamoja na vipimo vya vinasaba vilisaidia kumtambua na kumkamata mshukiwa huyo, lakini mkuu wa shirika la upelelezi wa ndani ya Marekani, FBI, Christopher Wray amesema bado kitisho hakijaondolewa kikamilifu.

”Inawezekana vifurushi vingine vya mabomu viko njiani, na vingine vitafuata,” amesema Wray katika mkutano na waandishi wa habari.

Afisa mmoja aliyezungumza na shirika la habari la Reuters amesema FBI inachunguza kujua ikiwa wapo watu wengine wanaohusika katika uhalifu huo, na hakuondoa uwezekano wa kuwakamata watu wengine.

Trump asema hawezi kuwajibishwa

Rais Donald Trump wa Marekani, ambaye kauli zake zinashutumiwa kuchochea migawanyiko

Akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa kampeni ya kisiasa katika jimbo la North Carolina, Trump amesema anatambua kwamba mshukiwa ni mfuasi wake, lakini hawezi kubebeshwa lawama za vitendo vyake.

Trump pia amevishutumu vyomba vya habari vya Marekani kukitumia kisa cha ”uhalifu wa mtu mmoja” kumshambulia yeye binafsi na kukihujumu cha cha Republican, kwa malengo ya kisiasa.

Tangu alipoanzisha kampeni yake ya kuwania urais mwaka 2016, na baada ya kushinda na kutwaa madaraka mwaka 2017, Trump amekuwa akitoa kauli zinazoshutumiwa kuchochea migawanyiko kwa misingi ya vyama, na kuyapa nguvu makundi ya kibaguzi na yanayopendelea matumizi ya nguvu na ghasia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *