MWILI wa aliyekuwa Waziri wa nchi ofisi ya Rais menejimenti ya Utumishi wa Umma na mgombea Ubunge wa jimbo la Ulanga mashariki kupitia-CCM– marehemu Celina Kombani kuagwa leo katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es salaam.
Kwa mujibu wa Taarifa zilizotolewa na Ofisi ya Bunge kupitia kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano zinaeleza kuwa baada ya Zoezi hilo kukamilika mwili wa marehemu utasafirishwa kwenda nyumbani kwa marehemu mkoani Morogoro ambapo utapokelewa na viongozi mbalimbali wa mkoa na maafisa kutoka serikalini.
Aidha taarifa zinasema kuwa ibada ya mazishi itafanyika kesho septemba 29 nyumbani kwake ikifuatiwa na Zoezi la kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa marehemu Celina Kombani kabla ya mazishi yatakayofanyika shambani kwake Lukobe nje kidogo ya mji huo.