Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amesema yuko radhi kwenda katika mahakama ya kimataifa ya ICC kwa kikao maalum kuhusu kesi inayomkabili.
Akiwahutubia wabunge mjini Nairobi,aliwaambia kuwa yuko tayarti kuhudhuria kikao maalum alichotakiwa kuhudhuria mjini Hague bila wasiwasi wowote.
Kenyatta alitakiwa na majaji wa mahakama hiyo kufika ICC tarehe 8 mwezi huu kufafanua madai kuwa serikali yake imekataa kushirikiana na mahakama hiyo hasa upande wa mashitaka kwa kukataa kuipatia ushahidi unaohitajika katika kesi inayomkabili.
Aliarifu bunge kuwa anajiamini mwenyewe kiasi cha kuwa tayari kufika mbele ya ICC na kwamba anajua hana hatia katika kesi inayomkabili.
Alisema Kenya ni nchi huru na kwamba haitawahi kuwa chini ya mamlaka nyingine yoyote.