Saudia yabanwa mbavu mauaji ya Khashoggi

Saudia yabanwa mbavu mauaji ya Khashoggi

Like
544
0
Monday, 22 October 2018
Global News

Nchi tatu zenye ushawishi mkubwa barani Ulaya, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zimelaani vikali mauaji ya mwandishi Jamal Khashoggi na kuitaka Saudi Arabia kutoa ufafanuzi wa kina haraka iwezekanavyo.

Taarifa ya pamoja ya mataifa hayo yanaitaka Saudia kutoa vielelezo vya kina juu ya madai kuwa Khashoggi aliuawa wakati akijaribu kupigana ndani ya ofisi za ubalozi mdogo wa Saudia jijini Istanbul, Uturuki.

Rais wa Marekani Donald Trump pia amebainisha kuwa “hakuridhishwa” na maelezo hayo ya Saudia.

Rais wa Uturuki Racep Tayyip Erdogan jana Jumapili ameahidi kudhihirisha ukweli wote juu ya tukio hilo.

Erdogan amesema atatoa maelezo juu ya sakata hilo kesho Jumanne atakapolihutubia bunge la nchi hiyo.

“Tunataka haki itendeke hapa, na juu ya jambo hili tutadhihirisha ukweli wote,” Erdogan aliuambia mkutano wa hadhara jijini Istanbul.

Khashoggi aliingia katika jingo la ubalozi mdogo mnamo tarehe 2 Oktoba kwa minajili ya kushughulikia karatasi zake muhimu kuhusiana masuala ya ndoa.

Awali mamlaka za Saudia zilidai kuwa alitoka, lakini mamlaka za Uturuki zilikanusha vikali na kusema kuwa wanaushahidi kuwa mwanahabari huyo alizuiliwa na baadae kuuawa na kisha mwili wake kukatwa vipande vipande.

Khashoggi alikuwa mkosoaji kinara wa sera za Mwanamfalme Mohammed Bin Salman na alihamia Marekani mwaka 2017 akihofia usalama wake.

Katika taarifa yao ya pamoja, nchi za Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zimesema kuwa zimeshtushwa na mkasa huo wakiamini hakuna sababu yeyote ile ya kutetea mauaji.

“Maelezo Zaidi na yenye ushahidi usiokuwa na chembe ya shaka yanahitajika… Hivyo basi, tunataka uchunguzi wa kina ufanyike na wahusika wote watambulike na hatua za kisheria zinastohili zichukuliwe kwa waliotenda unyama huu.”

Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia Adel al-Jubeir amekiambia kituo cha runinga cha Fox News cha Marekani kuwa Khashoggi aliuawa kwa makusudi na kikundi kilichojichukulia sheria mkononi.

Hata hivyo, al-Jubeir amekanusha taarifa kuwa mwanamfalme Bin Salman alijua mipango yote na kile kilichojiri ndani ya ofisi zao za ubalozi mdogo Uturuki. Pia amekiri makossa yamefanyika kwa kujaribu kuuficha ukweli.

Waziri huyo amesema uchunguzi wa kina unaendelea na watatoa vielelezo vyote vinavyohitajika kwa uwazi, “ukweli ni kwamba waliofanya ukatili huu walichupa mipaka ya kazi zao. Ni Dhahiri makosa yamefanyika na makossa makubwa Zaidi ni kujaribu kuuficha ukweli.”

Mamlaka za Saudia zinasema awali walitangaza kuwa Khashoggi alitoka nje ya jingo lao kwa sababu taarifa waliyopata kutoka kwa wawkilishi wao ilisema hivyo, na waliibadili mara tu walipotambua kuwa haikuwa ya kweli.

Mamlaka za Saudia zimekanusha Mwanamfalme Mohammed Bin Salman kuhusika katika mauaji ya Khashoggi.

Wadadisi na wakosoaji wa dola hiyo wanasema Saudia inabadili maelezo yake kutokana na shutuma zinazolekezwa kwao kutoka kwa jumuiya ya kimataifa.

Baadhi ya vyombo vya habari vya kimataifa vinanukuu vyanzo kutoka ndani ya serikali ya Saudia vikisema mwanamfalme Bin Salman ameshtushwa na ukubwa wa shutuma zinaolekezwa kwa nchi yake na hakutegemea suala hilo lingelikuwa kubwa kama ilivyo kwa sasa.

Shirika la habari la Reuters limeripoti jana kuwa kiongozi mmoja wa Saudia amewaambia kuwa Khashoggi aliuawa mara baada ya kukataa kurudishwa Saudia.

Baada ya kuuawa, shirika hilo linaripoti kuwa, mwili wake uliviringishwa kwenye zulia na kupewa mshiriki mmoja wa tukio hilo ambaye ni raia wa Uturuki ili akauteketeze.

Mmoja wa washiriki wa tukio hilo ambaye ni raia wa Saudia inadaiwa alivaa nguo za Khashoggi na kutoka nje ya ofisi hizo za ubalozi ili kupoteza ushahidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *