SERIKALI ISIPOTENGA BAJETI KUSAIDIA TFF KUINUA SOKA, TANZANIA ITAENDELEA KUWA POMBE YA NGOMANI KIMATAIFA

SERIKALI ISIPOTENGA BAJETI KUSAIDIA TFF KUINUA SOKA, TANZANIA ITAENDELEA KUWA POMBE YA NGOMANI KIMATAIFA

Like
278
0
Monday, 06 July 2015
Slider

Na Omary Katanga.

Hakuna ubishi kwamba nchi yeyote duniani yenye dhamira ya kweli ya kuwa na maendeleo katika michezo, serikali ni lazima iweke nguvu yake ya fedha kwa asilimia 50 hadi 80 kusaidia mpango huo.

Lakini inashangaza kuona katika nchi yetu shirikisho la mpira wa miguu TFF linalia kila kukicha kutokana na kukabiliwa na ukata wa fedha,hali inayocheleweshwa maendeleo ya sekta ya mpira wa miguu ambayo TFF inadhamana kubwa ya kusimamia.

Awamu ya rais Leodiga Tenga alipokuwa TFF alianzisha wimbo wa kuiomba serikali iweke bajeti maalum kusaidia kuinua mpira wa miguu kwa kuwekeza katika program za vijana,lakini wimbo huo unaoendelea kuimbwa na rais wa sasa Jamal Malinzi,inaonesha bado haujapenya masikioni mwa serikali.

Kwa sasa Tanzania inajitayarisha kushiriki michuano ya kuwania kufuzu kwa fainali za afrika kwa vijana (U-17),zitakazofanyika nchini Madagascar mwaka 2017,kwa kuwaandaa vijana wenye umri chini ya miaka 15 (U-15) ambao ndio watatumika kuiwakilisha nchini katika michuano hiyo wakati utakapofika.

Hivi karibuni kikosi hicho (U-150 kinachonolewa na kocha Bakari Shime,kimerejea jijini kutoka mkoani Mbeya kilipokwenda kujifua kwa kucheza mechi mbili za kujipima nguvu ,lakini kutokana na uhaba wa fedha kambi yake imevunjwa  mpaka watakapokutana tena mwisho wa mwezi huu na kuanza safari ya  kuelekea visiwani zanzibar kwaajili ya michezo mingine  ya kirafiki.

Alisikika rais Malinzi akisema hadharani kuwa angependa kuona vikosi vyote vya taifa vya vijana vinakuwa na kambi endelevu,lakini hali ya ukosefu wa fedha inakwamisha mipango hiyo na kuiomba serikali kuweka huruma yake mbele na kutumia dhamana iliyonayo kwa wananchi wake kusaidia kwa nguvu zote maendeleo ya mpira wa miguu,ili kuwa na timu za taifa imara zitakazoleta ushindani kwa mataifa mengine.

Ubovu wa timu yetu ya taifa Taifa Stars ilionao kwa kipindi kirefu kinasababishwa na kukosa wachezaji wanaoweza kushika nafasi za wale wa zamani ambao wamestaafu na wengine wanaoelekea kutengana na soka baada ya mwili na akili zao kukosa maarifa na ubunifu mpya uwanjani.

Kwa hali hii wala tusitegemee kuwepo na mabadiliko makubwa kwa Stars kwa kuendelea kuwatumia wachezaji walewale hata kama tutabadilisha makocha toka mataifa mbalimbali,na badala yake mabadiliko hayo yanaweza kuonekana endapo taifa litakuwa na hazina kubwa ya wachezaji watakaozalishwa kupitia program za vijana.

Endapo  serikali itaendelea kuweka pamba masikioni kukataa kusikiliza kilio cha kuwekeza katika program za soka kwa vijana,basi tanzania itaendelea kuitwa majina ya kukarahisha,kama Kichwa cha mwendawazimu,Pombe ya ngomani nk.

Nimalizie kwa kuwatakia kila la kheri wapiganaji wetu wa Taifa Stars walikunywa maji ya bendera,katika kibarua chao kigumu leo jioni mbele ya Uganda Cranes huko Kampala,katika mchezo wa marudiano kusaka tiketi ya CHAN,(Nimeweka silaha chini kuiunga mkono Taifa Stars)

Mwisho.

 

 

 

Comments are closed.