ILI kuhakikisha kuwa wananchi wa Tanzania wananufaika na rasilimali za madini mbalimbali pamoja na gesi iliyogunduliwa, Serikali imeanza kutoa mafunzo kwa wataalam kutoka taasisi za serikali watakaohusika na upitiaji wa mikataba yote ya shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini, gesi na mafuta kabla ya kusainiwa.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nishati na Madini mheshimiwa George Simbachawene katika uzinduzi wa warsha kuhusu dira mpya ya madini Afrika iliyofanyika mjini Morogoro.
Warsha hiyo ya siku tatu iliyoandaliwa na Wizara ya Nishati na Madini imewakutanisha wataalam kutoka taasisi za serikali ikiwa ni pamoja na Ofisi ya Makamu wa Rais, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha na Ofisi ya Rais- Tume ya Mipango.