Serikali kupitia, Programu ya Miundo mbinu ya Masoko, Uongezaji wa Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF), imetekeleza maombi 5 ambayo yanawasaidia wafugaji hao kuongeza thamani ya mifugo yao kupitia Soko la Kimkakati la mifugo Longido lililojengwa na Program hiyo.
Mwishoni mwa mwaka 2017, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira ,Kazi, Vijana na Watu wenye Ulemavu ) Mhe.Jenista Mhagama, alikuwa na ziara ya kukagua ujenzi wa soko hilo wilayani humo, ambapo baada ya ukaguzi alikutana na wafanyabiashara ya mifugo, ambao waliwasilisha maombi 5, ambayo yangeweza kuongeza Thamani Biashara za Mifugo na kutatua kero zote za wafanyabiashara wa mifugo wilayani humo.
“Serikali ya awamu ya tano imeamua kuwasikiliza watu wanyonge na ambao wanajituma kuchapa kazi, lakini pia lengo la Program ya MIVARF ni kuongeza kipato kwa wananchi hasa waishio vijijini, kwa mantiki hiyo nilimuelekeza Mratibu wa Program Kutekeleza maombi yao haraka sana ili wafugaji hawa wapate tija ya ufugaji kupitia soko hili” alisema Mhagama
Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa Mifugo wilayani Longido, Saruni Laizer amesema maombi waliyowasilisha serikalini ili waweze kupata tija ya mifugo kupitia soko la Kimkakati la Mifugo Longido yamefanyiwa kazi na Program ya MIVARF ndani ya miezi mitatu tangu wayasilishe, ikiwa ni; Mizani ya kupima mifugo, Maji ya kunyweshea mifugo, machinjio, Josho, pamoja na umeme.
“Tulihitaji maji hapa ili mifugo isije ikafa wakati inasubiri kuuzwa kwa kukosa maji, lakini umeme hapa ni muhimu kwani biashara zetu zinafanyika usiku, tayari hadi jenereta imeletwa kwa ajili ya kuhakikisha biashara haikwami kwa dharura yoyote ile, lakini mizani itasaidia kutowauza mifugo kwa kuangalia kwa macho bali kwa uzito wao” alisema Laizer