TAASISI ZA ELIMU YA JUU ZIIMARISHE MADAWATI YA MIKOPO

TAASISI ZA ELIMU YA JUU ZIIMARISHE MADAWATI YA MIKOPO

Like
482
0
Monday, 12 March 2018
Local News
 
Akifunga kikao kazi cha siku mbili kati ya Menejimenti ya HESLB na maafisa wanaosimamia madawati mikopo kutoka taasisi za elimu ya juu zaidi ya 70 mwishoni mwa wiki mjini Morogoro, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo amewataka viongozi wa taasisi hizo kuhakikisha maafisa wao wana vitendea kazi vya uhakika na wanapata ushirikiano wa kutosha.
Madawati hayo ya mikopo yalianzishwa mwaka 2011 katika taasisi zote za elimu ya juu kufuatia maelekezo ya Serikali ili kuongeza ufanisi katika kusimamia shughuli za utoaji mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi.
“Kila mdau kwenye utoaji wa mikopo ya elimu ya juu ana wajibu wake, Serikali inatoa fedha kwa wakati na menejimenti za taasisi za elimu ya juu ni wajibu wao ni kuimarisha wadawati ya mikopo yanayowahudumia wanafunzi kwa kuwawezesha ili ninyi maafisa mnayoyasimamia mtoe huduma nzuri kwa wanafunzi … mpewe ushirikiano na vitendea kazi,” alisema Dkt. Akwilapo wakati akifunga kikao kazi hicho kilichofanyika Alhamisi na Ijumaa ya wiki iliyopita (Machi 8-9, 2018).
Dkt. Akwilapo aliwakumbusha maafisa hao kuwa wao ndiyo watu wanaokutana na wanafunzi kwa mara ya kwanza huko vyuoni na kwamba ni muhimu wakatoa huduma bora kama Serikali ilivyotarajia wakati inatoa maelekezo ya kuanzishwa kwa madawati hayo.
Pamoja na kuimarisha madawati ya mikopo, Katibu Mkuu pia amazitaka taasisi kuhakikisha fedha za mikopo ya wanafunzi zinazopelekwa vyuoni zinawafikia wanafunzi kwa wakati kama ilivyokusudiwa na pale ambapo mwanafunzi hayupo chuoni, zirejeshwe kwa Bodi ya Mikopo haraka kama miongozo inavyotaka.
Lengo la kikao kazi
Akizungumza kabla ya Katibu Mkuu, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru alisema HESLB huandaa kikao kazi kama hicho mara moja kila mwaka ili kujadiliana kwa pamoja kuhusu utendaji kazi wetu kwa lengo la kuongeza ufanisi katika kutoa huduma kwa wanafunzi na wadau wengine.
Bw. Badru aliongeza kuwa katika kikao kazi cha mwaka huu, mada kadhaa ziliwasilisha na kujadiliwa. Mada hizo ni Mafanikio na Changamoto za utoaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2017/2018 na Mipango kwa 2018/2019; Taratibu na Nyaraka Muhimu zinazotakiwa ili kupanga na kutoa mikopo kwa wakati; Wajibu na Sifa za Ofisa Mikopo anayesimamia Dawati la Mikopo; Taratibu za Urejeshaji wa Mikopo; na Maboresho makubwa yanayoendelea katika mifumo ya TEHAMA ya HESLB.
“Pamoja na mada hizi, kwa mara ya kwanza mwaka huu tumewapa washiriki wote fomu maalum za kutoa tathmini yao kuhusu utendaji wetu kama HESLB na maoni yao tutayafanyia kazi ili kuboresha utendaji kazi wetu,” alisema Bw. Badru na kuongeza kuwa kikao kazi hicho pia kimehudhuriwa na Mwenyekiti wa Shirikisho la Serikali za Wanafunzi wa Vyuo Vikuu (TAHLISO) Bw. George Mnali na Naibu Katibu Mkuu wake Bw. Ali Abdallah Simba.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAHLISO aliishukuru HESLB kwa kuwaalika katika kikao kazi hicho kwa mara ya kwanza na kuiwezesha taasisi yake kukutana na maofisa hao ambao ndiyo watu wa kwanza kuwahudumia wanafunzi katika taasisi za elimu ya juu.
“Sisi tumefarijika sana kukutana na watendaji wa HESLB na maafisa mikopo uso kwa uso… ni matumaini yetu kuwa hatua hii itasaidia kuboresha uhusiano na kutatua kero za wanafunzi,” alisema Bw. Mnali.
Taasisi tano zakabidhiwa ngao
Wakati huohuo, Katibu Mkuu Dkt. Akwilapo alikabidhi ngao kwa taasisi tano bora za elimu ya juu kutambua huduma bora na ushirikiano unatolewa na taasisi hizo na maafisa wake kwa HESLB. Taasisi zilizokabidhiwa ngao hizo Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Dar es Salaam (DUCE); Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Abdulrahman Al-Sumait (SUMAIT); Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE); Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Sebastian Kolowa (SEKOMU) na Chuo Kikuu Kishiriki cha Marian (MARUCO).
“Tumefanya tathmini yetu ya ndani katika maeneo matano na kujiridhisha kuwa katika mwaka huu wa masomo, maafisa wanaosimamia madawati katika taasisi hizi wametekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi,” alisema Bw. Badru katika siku ya pili ya kikao kazi hicho.
Aliongeza kuwa maeneo yaliyofanyiwa tathimini ni Uwasilishaji wa nyaraka sahihi kwa wakati kwa Bodi ya Mikopo; Utoaji wa huduma kwa wanafunzi waliopo vyuoni na utunzaji wa kumbukumbu za wanafunzi ambazo ni muhimu katika kuwezesha HESLB kuandaa malipo na kuyafikisha katika vyuo kwa wakati.
RC Dkt. Kebwe afungua kikao kazi
Kikao kazi hicho kilifunguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Stephen Kebwe siku ya Alhamisi (Machi 9, 2018) ambaye, pamoja na mambo mengine alirejea nia ya Serikali kuona wanafunzi wote wenye sifa za kujiunga na taasisi za elimu ya juu lakini hawana uwezo wa kumudu gharama, wanapata mikopo kutoka Serikali.
HESLB ni taasisi ya Serikali iliyoanza kazi zake rasmi mwezi Julai, 2005. Majukumu yake makubwa ni kutoa mikopo kwa watanzania wahitaji na wenye sifa za kujiunga na taasisi za elimu ya juu na pia kukusanya mikopo ya elimu ya juu iliyoiva kutoka kwa wanufaika.

Comments are closed.