IMEELEZWA kuwa takribani waandishi wa habari 60 kote ulimwenguni waliuawa katika mwaka wa 2014 wakiwa kazini au kwa sababu ya kazi zao, na asilimia 44 ya wanahabari waliuawa kwa makusudio.
Ripoti mpya ya Kamati ya Kuwalinda Waandishi wa Habari yenye makao yake mjini New York, Marekani, imesema idadi kubwa ya wale waliouawa ni waandishi wa habari wa kimataifa, japo kuwa idadi kubwa zaidi ya wanahabari wanaotishiwa inaendelea kuripotiwa katika nchi mbalimbali.
Karibu wanahabari 17 wameuawa nchini Syria ambako mgogoro wa vita umedumu kwa karibu miaka minne. Aidha migogoro ya Ukraine na Urusi, na mapigano yaliyotokea katika Ukanda wa Gaza kwa siku 50 baina ya Waisrael na Wapalestina, pia yalisababisha vifo vya wanahabari kadhaa.