Rais donald Trump amesema siku ya Jumamosi(20.10.2018) kwamba Marekani itajitoa kutoka mkataba wa enzi za vita baridi ambao unafuta aina ya silaha za nyuklia kutokana na ukiukaji unaofanywa na Urusi.
Hatua hiyo imeelezwa na afisa mmoja wa Urusi kuwa ni jaribio hatari la kuibana nchi hiyo.
Mkataba unaojulikana kama Intermediate-Range Nuclear Forces Treaty, uliojadiliwa na kufikia makubaliano wakati wa utawala wa rais Ronald Reagan na kiongozi wa Urusi wakati wa enzi za Umoja wa kisovieti Mikhail Gorbachev mwaka 1987, unataka kuondolewa kabisa kwa makombora ya kinyuklia ya masafa mafupi na kati pamoja na makombora ya bara hadi para kwa nchi zote.
“Urusi kwa bahati mbaya, haijatimiza makubaliano hayo kwa hiyo tutasitisha makubaliano hayo na tutajitoa,” Trump aliwaambia waandishi habari baada ya mkutano wa hadhara mjini Nevada.
Washington inaamini serikali ya mjini Moscow inatengeneza na imeweka mfumo wa kurusha makombora wa ardhini ambao ni ukiukaji wa mkataba huo wa INF ambao ungeweza kuruhusu Urusi kufanya mashambulio ya nuklia katika mataifa ya Ulaya muda mfupi sana wakitaka.
Urusi yakana
Urusi imekuwa ikikana ukiukaji wowote kama huo.
Trump amesema Marekani itatengeneza silaha hadi pale Urusi na China zitakapokubali kusitisha utengenezaji.
China haimo katika mkataba huo na imewekeza kwa kiasi kikubwa katika makobora ya masafa marefu kama sehemu ya mkakati wa kuzuwia kuingiliwa katika maeneo yake, wakati mkataba wa INF umepiga marufuku Marekani kuwa na makombora ya masafa marefu yanayorushwa kutokea ardhini ama makombora yenye uwezo wa kurushwa kwa umbali wa kilometa 500 na 5,500.
Mshauri wa usalama wa taifa wa Trump , John Bolton , atakwenda Moscow wiki ijayo.
Naibu waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi , Sergei Ryabkov, katika matamshi yaliyoripotiwa na shirika la habari la Urusi TASS, amesema hatua ya Marekani kuchukua uamuzi wa kujitoa bila makubaliano na upande wa pili “itakuwa hatua ya hatari sana.”
Ryabkov pia amenukuliwa akisema kwamba ni Marekani na Urusi ambazo zinashindwa kutekeleza mkataba huo.
Amesema utawala wa Trump unatumia mkataba huo katika jaribio la kuikandamiza serikali ya Urusi, na kuuweka usalama wa dunia katika hatari.