Waandishi wa habari hata hivyo wamearifu kwamba kwenye majimbo ya nchi hiyo ya Afrika ya kati yanayotumia lugha ya Kifaransa zoezi la uchaguzi limeendelea bila ya mushkeli wowote. Rais Paul Biya anawania muhula wa saba huku nchi yake ikiwa inakumbwa na vurugu katika mikoa inayotumia lugha ya Kiingereza. Biya amekuwa madarakani tokea mwaka 1982 na ameahidi kuumaliza mgogoro ambao umesababisha vifo vya watu zaidi ya 400 Kusini-magharibi na Kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo.
Upinzani uliogawanyika umeshindwa kusimamisha mgombea mwenye nguvu ya kuweza kuchuana na Biya mwenye umri wa miaka 85 na mmoja wa watawala wa muda mrefu zaidi barani Afrika. Hayo ni kwa sababu wapinzani wawili wakuu nchini Cameroon waliounda muungano wa kwanza wa vyama vya upinzani mnamo 1992, walishindwa kufikia makubaliano na vyama vingine vya upinzani ili kuunda ushirikiano wenye nguvu dhidi ya rais Biya.
Rais Biya na mke wake Chantal, walipiga kura zao kwenye shule ya umma ya Bastos iliyo katika mji mkuu wa Yaounde chini ya ulinzi mkali. Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Democratic Front Joshua Osih alipiga kura katika mji wa Douala na ametoa mwito wa kuzingatiwa uwazi katika zoezi la kuhesabu kura.
Raia wa Cameroon wapatao milioni 6.5 wameshiriki katika uchaguzi huo huku Rais Paul Biya akitarajiwa kushinda awamu nyingine ya uongozi katika uchaguzi huo wa rais. Ushindi wa Biya hata hivyo hautakuwa na mamlaka yenye nguvu kwavile wananchi wengi wameyahama makazi yao katika eneo linalozungumza Kiingereza ambalo limekumbwa na ghasia.