Maelfu ya waandamanaji wamekita kambi nje ya makao makuu ya jeshi nchini Sudan, wakimtaka rais Omar al-Bashir ajiuzulu.
Inavyoonekana wanatarajia mapinduzi ya ndani ya nchi, wakiliomba jeshi kumtimua Bashir na kufungua njia ya kupatikana serikali ya mpito.
Ni maandamano makubwa dhidi ya Bashir tangu kuzuka ghasia mnamo Desemba mwaka jana.
Bashir amekataa kuondoka, akieleza kwamba wapinzani wake wanastahili kutafuta uongozi kupitia uchaguzi. Jeshi halijaingilia kati.
Maafisa wa usalama wamefyetua gesi ya kutoa machozi kuwatimua wandamanaji nje ya makao hayo makuu katika mji mkuu, Khartoum.
Maandamano haya yanaadhimisha miaka 34 ya mapinduzi yaliouondoa utawala wa rais Jaafar Nimeiri.
Katika maandamano ya nyuma, wamettumia pia guruneti na silaha za moto zikiwemo risasi. waandamanaji kadhaa wameuawa .
Siku ya Jumamosi, mwandamanaji mmoja alifariki katika mji wa Omdurman, polisi wanasema.
Waziri wa habari nchini Sudan amethibitisha mipnago ya serikali kutatua mzozo kupitia mazungumzo na kupongeza vikosi vya usalama.
Ni wazi kwamba yanayodhihirika katika mji mkuu Khartoum yanardhirisha. Umati kama huuu haujawahi kushuhudiwa kwa miongo kadhaa.
Lakini kumeshuhudiwa vifo kadhaa na kuna uwezekano wa kuwepo msako mkali kwa hivi sasa.
Na hata iwapo rais Bashir atajiuzulu hakuna uhakika kwamba nafasi yake itachukuliwa na serikali itakayokuwa na uwakilishi wa wengi kama wanavyotaka waandamanaji.
Serikali za utawala wa nguvu katika karne ya 21 barani Afrika zimeadimika na kutoa taswira ya mabadiliko lakini inayotoa maana finyu.
Kinachofichuka sasa huenda ni sehemu ya ushindani wa kisiasa usiotarajiwa wa muda mrefu zaidi.
Mwandishi habari Mohamed Ali Fazari, aliyekuwepo katika umati wa waandamanaji mjini Khartoum, anasema waanadamanaji hao wanaliomba jeshi lishirikiane na raia dhidi ya serikali.
Umati ulipiga kelele ukisema “uhuru, uhuru, haki – jeshi moja, watu wamoja”,
Kiini cha maandamano hayo awali kilitokana na gharama kubwa ya maisha lakini sasa ni ya kumshinikiza rais Bashir ambaye amekuwa madarakani kwa takriban miaka 30 sasa, ajiuzulu.
Uchumi wa Sudan umeathirika kwa muda mrefu na vikwazo vya Marekani kwa zaidi ya miaka 20 iliyopita inayoishutumu Khartoum kwa kufadhili makundi ya kigaidi.
Mnamo Desemba mwaka jana serikali ya Sudan ilitangaza kwamba bei ya mafuta na mkate itapanda
Katika mwaka uliofuata uamuzi huu, gharama ya maisha ilipanda huku pauni ya Sudan ikashuka thamani kwa kiasi kikubwa.
Tangazo la kupanda kwa bei ya bidhaa hizo ilichangia kuzuka maandamano, yaliogeuka kuwa shinikizo dhidi ya Bashir ajiuzulu.
Utawala wake umegubikwa kwa shutuma za uikukaji wa haki za binaadamu.
Mnamo 2009 na 2010, mahakama ya kimataifa ya jinai (ICC) ilimshtaki kwa makosa ya uhalifu wa kivita, mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya binaadamu. Waranti wa kumkamata umetolewa.
Usalama umeimarishwa pakubwa mitaani huku gesi za kutoa machozi zikitumika kiholela na ripoti za kuwepo ghasia zikiwa ni jambo la kawaida.
Maafisa nchini humo wameshutumiwa kwa kuwakamata wanaharakati maarufu na kuwalenga matabibu , jambo ambalo idara ya ujasusi inakana.
Maafisa wanasema watu 32 wamefariki katika ghasia zinazohusiana na maandamano kufikia sasa, lakini shirika la Human Rights Watch linasema huenda idadi hiyo ni 51.
Kundi la kutetea haki za binaadamu Physicians for Human Rights linasema lina ushahidi wa mauaji, na unyanyasaji wa waandamanaji wa amani na matabibu waliokuwa wakiwashughulikia.
cc;BBCswahili