Wabunge Kenya watofautiana kuhusu matamshi ya ‘chuki’ ya Charles Kanyi ‘Jaguar’

Wabunge Kenya watofautiana kuhusu matamshi ya ‘chuki’ ya Charles Kanyi ‘Jaguar’

Like
687
0
Thursday, 27 June 2019
Global News

Matamshi ya mbunge wa Starehe nchini Kenya Charles ‘Jaguar’ Kanyi kuhusu kuwatishia raia wa kigeni wanaofanya kazi nchini Kenya yaliwasilishwa mbele ya kikao cha bunge ili kujadiliwa.

Hatua hiyo inajiri huku Mbunge huyo akizuiliwa katika kituo cha polisi usiku kucha ambapo anasubiri kuwasilishwa mahakamani siku ya Alhamisi.

Kulingana na mtandao wa runinga ya Citizen nchini Kenya, licha ya wabunge wengi kushutumu jinsi ambavyo bwana Jaguar alitoa hoja yake , baadhi yao walikubaliana kwamba kuna swala tata kuhusiana na raia wa kigeni ambalo lilihitaji kuangaziwa.

Kulingana na mtandao huo swala hilo liliwasilishwa na mwenyekiti wa kamati ya Ulinzi na Uhusiano wa kigeni Katoo Ole Metito katika taarifa yake, akithibitisha kwamba raia wa kigeni hususan kutoka Jumuiya ya Afrika mashariki wana uhuru wa kufanya biashara nchini Kenya.

”Tunashutumu sana matamshi yoyote ya chuki yanayokiuka msimamo huu unaotuleta sisi pamoja kama taifa na kuthibitisha sera ya kuwakaribisha raia wote wa kigeni”, alisema mbunge huyo wa Kajiado kusini.

Matamshi yake yaliungwa mkono na mbunge wa Suba Kaskazini John Mbadi ambaye aliwarai wabunge wenzake kutotoa matamshi mbele ya umma kwa lengo la kujitafutia umaarufu na badala yake kuchukua tahadhari.

”Kama bara, tunahitaji kukuza uwiano katika mipaka yetu ili kutafuta ajira; Wakenya wako huru kwenda Tanzania kufanya biashara iwapo biashara hiyo ni halali”, alisema Mbadi.

Hatahivyo kiongozi wa walio wengi bungeni Aden Duale, ambaye pia alishutumu matamshi hayo ya mbunge huyo wa Starehe alisema kwamba Kenya sio jaa la raia wa kigeni na bidhaa zao, kulingana na mtandao wa Citizen kenya.

Kulingana na mbunge huyo wa Garissa mjini, Bunge pamoja na serikali zinafaa kuwalinda wananchi wa kawaida kutopoteza kazi kwa idadi kubwa ya raia wa kigeni waliomo nchini.

Mbunge huyo alitaja mfano ambapo wataalam kutoka Kenya kama vile afisa wa kampuni ya Safaricom Sylvia Mulinge alinyimwa fursa ya kufanya kazi katika taifa jirani la Tanzania, akiongezea kuwa Kenya pia inafaa kutokubali maswala mengine.

“Lazima ukweli usemwe; Unapoona biashara ya uchuuzi ikichukuliwa na raia wa taifa jingine tuna jukumu la kuwalinda watu wetu. Hawa wabunge hawafai kusahau kwamba kuku wetu walichomwa Tanzania , ng’ombe wetu walipigwa mnada Tanzania”, alisema Duale.

”Leo chini ya utawala uliopo Tanzania Wakenya hawawezi kufanya biashara, kwa nini bidhaa zetu haziingi Tanzania? Kwa sababu wametuwekea kodi ya juu”.

Duale aliwataka wabunge kutolichukulia swala hilo na hisia, bali kuchukua tahadhari wanapochukua jukumu lao la kuwalinda raia wa kawaida.

”Kama bunge ni lazima tuamue na kuleta sheria zitakazolinda biashara zetu. Munaweza kumshutumu Jaguar, lakini leo ndiye mbunge maarufu zaidi katika eneo bunge lake”, aliongezea Duale.

Nae mbunge wa Ugenya David Ochieng, kwa upande wake aliilaumu idadi kuu ya raia wa kigeni wanaofanya biashara nchini Kenya kwa kushindwa kwa serikali kuidhinisha sera yake.

”Katika uchumi wa leo , ni rahisi kununua bidhaa kutoka mataifa jirani kama vile Tanzania na Uganda na kuleta Kenya. Sio kwamba hatuna sheria, ni swala la utekelezwaji na ufisadi. Tunwaruhusu watu kuingia nchini na kuanza kuuza vitu barabarani. Huwezi kuwalaumu Watanzania kwa kufanya hivyo ni kwa sababu ya mfumo wetu ambao ni dhaifu”, alisema Ochieng’.

”Hatuwakagui watu wanaoingia nchini. Watanzania wanafanya kazi yao, ndio sababu wanaweza kujua kwamba Mulinge hakuhitimu kufanya kazi Tanzania.

Hatahivyo Mbunge huyo alishutumu matamshi ya Jaguar , huku akilitaka bunge hilo kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya wabunge wanaoharibu jina la taifa hilo katika ulingo wa kimataifa.

Tayari ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai kupitia ukurasa wake wa Twitter imesema mbunge huyo anashikiliwa kwa tuhuma za kuchochea ghasia.

Katika kanda ya video iliosambazwa pakubwa nchini Kenya na katika nchi jirani Tanzania, mbunge huyo alisema hawatokubali watu wa nje waje kuendesha biashara nchini humo.

Comments are closed.