Wanawake wajasiriamali wanaoshughulika na kubangua korosho nchini wamelalamikia mpango mpya uliotangazwa na rais Magufuli ambapo sasa jeshi la nchi litasimamia biashara shughuli hiyo.
Wanawake hao wanasema kuwa hatua hiyo itawanyima fursa ya ununuzi wa kiwango cha kawaida kwa lengo la biashara ndogo ndogo kwani, wana wasiwasi kwamba huenda jeshi likabadili kabisa mfumo wa uuzaji korosho tofauti na walivyo zoea.
Hapo jana ikiwa ni kabla ya muda uliowekwa kwa wafanyabiashara kujiorodhesha ili wanunue korosho ya wakulima mkoani Mtwara, rais alibadili mawazo yake na kuamua kwamba wafanya biashara hao hawatanunua tena korosho hiyo, akihoji kwamba walikuwa wapi.
“Yani huu mpango ambao rais ameuweka katika uuzaji wa korosho Mtwara kusimamiwa na jeshi, sisi wafanyabiashara wadogo kiukweli wametuangusha”, amedai mmoja wa wanawake ambaye ni maarufu kwa biashara hiyo.
“Mimi ni mjasiriamali mdogo ambaye nnanunua gunia moja au mbili katika kipindi cha msimu wa korosho , nabangua na kuuza. Sasa wameweka usimamizi wa jeshi , nitanunua wapi? Nina miaka 15 ninafanya hii shughuli nnaendesha maisha na nnasomesha watoto”… amelalamika mjasiriamali mwingine mwanamke.
Leo ni siku ya pili Baada ya serikali kukabidhi Jeshi la nchi hiyo, kuratibu shughuli za ununuzi wa korosho katika mkoa ulioko Kusini mwa nchi hiyo, Mtwara.
Hatua hiyo inafuatia Rais John Magufuli kusitisha mpango wa makampuni kununua zao hilo kwa kile alichodai wamekuwa na bei hazina tija kwa wakulima .
“Kiukweli nimevurugwa kwa msimamo huu uliowekwa, kwa sababu sisi ni wajasiriamali wadogo ambao hatuna uwezo wa kununua tani moja, tani mbili ..tunajikwamua tu kidogo kidogo.
Wanasaidiwa wakulima lakini sisi wajasiriamali wadogo wadogo tutaishije?”
Kwa sasa korosho zinauzwa kwa gharama ya shilingi 3,300 badala ya shilingi 3000 za kitanzania ambayo ni sawa na dola 1.43.
Rais amesema anataka kuhakikisha maelfu ya wakulima wanapata faida kwa mazao yao na kuhakikisha kipato kutokana na usafirishaji wa korosho katika mataifa ya nje.
Lakini wakosoaji wanasema huenda ni hatua ya kujaribu kutafuta uungwaji mkono katika eneo la Mtwara, eneo lililo ngome ya upinzani.
Mwansiasa wa upinzani Zitto Kabwe amesema serikali inastahili kupata ridhaa ya bunge kununua korosho hizo.
Kadhalika rais Magufuli ameivunjilia mbali bodi ya usimamizi wa zao la korosho Tanzania na kutegua uteuzi wa mwenyekiti wake, Anna Abdallah.