WAKAZI wa Mkoa wa Lindi wametakiwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura ili waweze kushiriki kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika mwishoni mwa mwaka huu.
Rai hiyo imetolewa na Mjumbe wa Kamati kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jerry Silaa wakati akiongea kwenye kilele cha sherehe za kutimiza miaka 38 ya chama hicho mkoani Lindi zilizofanyika katika tawi la Mnazi Mmoja lililopo kata ya Mingoyo wilaya ya Lindi mjini.
Silaa mbaye pia ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala amesema iwapo mtu atajiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura atashiriki katika uchaguzi mkuu ujao hivyo basi wakati ukifika ni jukumu la mabalozi kuwahimiza wananchi kujiandikisha ili wasipoteze haki yao ya msingi ya kupiga kura.