Takriban watu 40 wamefariki dunia kufuatia mafuriko yaliyosababishwa na mvua nyingi katika jimbo la Katsina, kaskazini mwa Nigeria.
Maafisa nchini humo wamesema mafuriko hayo yametokea katika eneo lililompakani na Niger. Miili 22 tayari imezikwa na mingine 18 imerejeshwa kutoka Niger, ambako miili hiyo ilisombwa na maji.
Mvua iliyonyesha siku ya Jumapili usiku na kunyesha mfululizo kwa saa nne, ilisababisha mafuriko makubwa katika mji wa Jibia.
Mafuriko hayo pia yalisababisha mto ulioko jirani na eneo hilo kuvunja kingo zake na maji kutawanyika katika makaazi ya watu.
Watoa huduma za uokoaji bado wanaendelea kuitambua miili ya waliokufa.
Takriban makaazi laki mbili na magari elfu mbili yaliharibiwa na mafuriko hayo.
Baadhi ya watu waliopoteza makaazi na mali zao, wamejihifadhi katika shule ya msingi iliyopo kwenye eneo hilo.