Zaidi ya watu 40 wafariki baada ya bwawa la Patel kuvunja kuta zake Nakuru Kenya

Zaidi ya watu 40 wafariki baada ya bwawa la Patel kuvunja kuta zake Nakuru Kenya

Like
592
0
Friday, 11 May 2018
Global News

mafuriko

Zaidi ya watu 40 wamefariki na maelfu wengine wameachwa bila ya makaazi wakati bwawa moja mjini Nakuru nchini Kenya lilipovunja kuta zake Jumatano usiku.

Shirika la kupambana na majanga nchini Kenya linasema watu wengine wengi hawajulikani waliko kufikia sasa.

Eneo hilo la Solai katika kaunti ya Nakuru Kenya, lina mabwawa saba yanayotumika katika kilimo cha umwagiliaji.

Waziri wa mambo ya ndani Kenya Fred Matiang’i amesema serikali imeanzisha uchunguzi kubaini uthabiti wa mabwawa mengine sita yaliosalia.

Maafisa wa uokozi kutoka mashirika tofauti nchini wamekuwa katika jitihada za kutafuta miili ya watu waliokufa kutokana na mkasa huo.

Mamia ya makaazi ya watu yaliosombwa na maji

Mapema leo Ijumaa kulikuwa na hisia ya wasiwasi wakati taarifa zilisambaa katika mitandao ya kijamii kwamba bwawa la pili limepasuka katika eneo lilo hilo.

Msemaji katika wizara ya mambo ya ndani Kenya Mwenda Njoka hatahivyo amekanusha taarifa hizo katika ujumbe aliotuma kwenye Twitter akieleza kwamba maji hayo yametokana na shughuli za wahandisi wanaopunguza kiwango cha maji yaliojaa katika mabwawa mengine katika eneo hilo.

Njoka amesema hatua hiyo imefanywa chini ya udhibiti wa wataalamu ili kuruhusu ukaguzi wa mabwawa hayo.

Bwawa la Patel mjini Nakuru katika mkoa wa bonde la ufa lilivunja kuta zake Jumatano usiku na kusomba mamia ya nyumba za wakaazi waliokuwa karibu na eneo hilo.

mafuriko

Walioshuhudia wanasema walisikia mshindo mkubwa kabla ya mawimbi makubwa kuyasomba makaazi na mashamba ya watu yenye umbali wa takriban kilomita mbili, eneo ambalo watu wengi wanaishi na kufanya kazi.

Jitihada za kuwatafuta manusuru zilisitishwa jana usiku kutokana na kutanda giza, hatahivyo inahofiwa kwamva huenda idadi ya watu waliofariki ikaongezeka wakati jitihada zikiendelea leo kuwatafuta manusura.

Huu ni mkasa wa kwanza wenye ukubwa wa aina hii kuwahi kushuhudiwa Kenya.

Zaidi ya watu 2000 wameachwa bila ya makaazi.

Wakaazi wanasema watu wengine zaidi hawajulikani waliko.

Bwawa hilo la Patel ni mojawapo ya mabwawa matatu yanayomilikiwa na mkulima mmoja mkubwa katika eneo hilo.

Inaarifiwa kwamba kuta zake zilibomoka kutokana na maji mengi yaliokusanyika kufutia mvua kubwa inayoendelea kunyesha nchini.

Viongozi wa eneo hilo sasa wanataka kujuwa iwapo mkulima huyo ana kibali kilichomruhusu kujenga mabwawa hayo, huku kukiwa na wasiwasi kuhusu hali ya mabwawa mawili yaliosalia ambayo pia yanatajwa kuwa yamejaa.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *