WAZIRI wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier ameionya Urusi dhidi ya kuchochea zaidi mgogoro wa Ukraine, akisema mashambulizi ya waasi kwenye mji wa Mariupol yatakuwa ukiukwaji wa wazi wa makubaliano ya amani yalioungwa mkono na jamii ya kimataifa.
Katika mahojiano na gazeti linalosomwa na watu wengi zaidi nchini Ujerumani la Bild, toleo la leo Jumatatu, Steinmeier ambaye yuko nchini Kenya akikamilisha ziara yake ya mataifa matatu ya Afrika, amesema hatua yoyote ya kusonga mbele kwenye mji huo itakuwa ukiukaji wa makubaliano ya Minsk.
Hapo Ijumaa, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alisema kuwa vikwazo vipya dhidi ya Urusi vitazingatiwa ikiwa makubaliano hayo ya amani yatakiukwa.