Theresa May amekitolea wito chama chake cha Conservative kumuunga mkono na kuiunganisha Uingereza. May amewataka wanachama hao kuunga mkono mpango wake kuhusu mchakato wa Uingereza kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya
Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May amekitolea wito chama chake cha Conservative kumuunga mkono na kuiunganisha Uingereza ambayo imegawanyika kutokana na tofauti za maoni zilizochochewa na mpango wake wa Uingereza kujiondoa kwenye umoja wa Ulaya.
Akizungumza mjini Birmingham katika hotuba yake ya kuufunga mkutano mkuu wa mwaka wa chama cha Conservative, May amewataka wanachama hao kuunga mkono mpango wake kuhusu mchakato wa Uingereza kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya maarufu kama Brexit na kukijenga chama chenye heshima na cha kizalendo. Mpango huo wa Brexit unajulikana kama ”Chequers”.
Amekikosoa chama cha upinzani cha Labour na kumshutumu kiongozi wake, Jeremy Corbyn kwa kukataa mapendekezo ambayo yaliwahi mara moja kuwaunganisha wanasiasa waliokuwa wamegawanyika. May amesema wanahitaji kuwa chama kwa ajili ya nchi nzima, na sio chama cha wachache, lakini kwa kila mmoja ambaye yuko tayari kufanya kazi kwa bidii.
”Na kuna sababu nyingine kwa nini tunahitaji kuungana pamoja. Tunaingia katika awamu ngumu ya mazungumzo. Mliona Salzburg, kwamba niliisimamia Uingereza. Tunachopendekeza ni changamoto kubwa kwa Umoja wa Ulaya, lakini kama tukiungana pamoja, najua tunaweza kupata makubaliano yenye tija kwa Uingereza.”