SHIRIKA la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema polisi katika mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Kinshasa, walifanya mauaji kadhaa katika operesheni iliyodumu miezi mitatu dhidi ya makundi ya kihalifu.
Shirika hilo limesema operesheni hiyo iliyopewa jina Likofi iliyozinduliwa Novemba mwaka uliopita ililenga kukomesha ongezeko la wizi wa kutumia silaha na uhalifu mwingine unaofanywa na makundi madogo yanayojulikana kama kuluna.
Katika ripoti iliyotolewa leo shirika la Human Rights Watch linasema polisi walioshiriki katika harakati hiyo waliwaua wanaume na vijana wasiopungua 51, wakati mwingine wakiwa bila silaha, nje ya nyumba zao au katika masoko.