Mambo muhimu ya kuhakikisha usalama wako mvua inaponyesha

Mambo muhimu ya kuhakikisha usalama wako mvua inaponyesha

Like
704
0
Thursday, 10 May 2018
Local News

Mvua kubwa imekuwa ikinyesha maeneo mengi Afrika Mashariki na kusababisha uharibifu wa mali na vifo.

Nchini Kenya, watu zaidi ya 10 wamefariki baada ya kusombwa na maji ya mafuriko

Wengi wao wamefariki wakisafiri kuelekea nyumbani au wakiwa kwenye magari wakijaribu kupitia maeneo yaliyofurika

Je, unaweza kujikinga vipi hasa ukiwa safarini?

Maafisa wa Mamlaka ya Taifa ya Usalama Barabarani (NTSA) pamoja na Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya wametoa ushauri ambao unaweza kukufaa sana wakati huu wa mvua.

Fahamu kwamba wakati wa kiangazi, vumbi, mchanga na taka za aina mbalimbali hurundikana barabarani. Mvua inaponyesha, husababisha barabara kuwa telezi na kwa hivyo ukiwa na gari ni muhimu kutoendesha gari lako kwa mwendo wa kasi kupindukia kwani gari likiteleza utashindwa kulidhibiti gari lako kwa urahisi.

Kwa sababu ya maji, huwa vigumu sana kupiga breki wakati wa mvua na hivyo hatari ya mwenye gari kumgonga anayetembea barabarani huwa juu. Unashauriwa kutoendesha gari kwa mwendo wa kasi.

Kwa sababu ya mvua, wapita njia mara nyingi hutembea wakiwa wameinamisha vichwa chini na huenda wasilione gari linapokaribia. Wenye magari wanashauriwa kuwa makini zaidi wanapofika kwenye vivuko barabarani au wanapomuona mtu akivuka barabara. Kwa wanaotembea kwa miguu, wanashauriwa kutumia vivuko vilivyotengwa na kuchukua tahadhari zaidi pia.

Kwa wenye magari, iwapo barabara imefurika maji, ni vyema kutafuta barabara nyingine ya kupitia badala ya kujaribu kupitia ndani ya maji. Huwa vigumu kukadiria kina cha maji barabara inapofurika.

Wakati mvua inaponyesha, wenye magari wanatakiwa kuwasha taa kuwawezesha kuona mbele na pia kutokaribia sana magari yaliyo mbele yao. Maji yanayorushwa na gari lililo mbele yanaweza kutatiza mwenye gari iwapo atakuwa karibu sana. Ushauriwa kufuata kanuni ya sekunde 3, hicho ndicho kipindi kinachochukuliwa na binadamu kuona jambo na kuchukua hatua. Usipofanya hivi, kufikia wakati unapoona aliye mbele yako amesimama na kuchukua hatua utakuwa tayari umesababisha ajali.

Breki za gari huathiriwa na maji, kwa hivyo unapoendesha gari eneo lenye maji, ni vyema kuendesha gari kwa mwendo wa polepole. Hii itaziwezesha breki kukauka.

Madereva wanashauriwa pia kutumia mikono yao miwili kudhibiti mwelekeo wa gari kuhakikisha wanadhibiti vyema gari.

Wapita njia, waendesha baiskeli na waendeshaji pikipiki wanashauriwa kuvalia mavazi yanayoweza kuonekana vyema au mavazi yanayoweza kuakisi mwanga. Haya yatamuwezesha mtu kuonekana na madereva na kumpungushia mtu hatari ya kugongwa.

Usiendeshe gari lako ndani ya maji yanayosonga, yawe kwenye mifereji au kwenye mto. Huwa vigumu sana kukadiria nguvu ya maji. Magari mengi husombwa na maji madereva wakijaribu kuvuka mito au wakitumia madaraja yaliyofurika maji. Mvua pia hudhoofisha madaraja, jambo ambalo huenda usifahamu. Daraja linaweza kubomolewa bila ufahamu wake wewe nawe ukaingia mtoni ukitarajia daraja bado lipo. Maji ya kina ya futi moja yanaweza kusomba gari lako. Kwa binadamu anayetembea, inchi sita za maji zinaweza kukusomba.

Ukiwa na gari lako, hakikisha vipangusia kioo vya gari lako vinafanya kazi. Hili litakuwezesha kupangusa kioo na kuona mbele unapokuwa barabarani.

Iwapo una gari na limeanza kuteleza, achilia mafuta na kulielekeza gari upande ambao unateleza. Ukianfanikiwa kudhibiti gari, anza kulainisha magurudumu tena na kurejea barabarani. Hakikisha kwamba unabaki kuwa tulivu na usichukue hatua yoyote ghafla.

Usiende kwa mwendo wa kasi. Iwapo una safari ya mbali, anza mapema kuhakikisha kwamba haukumbwi na shinikizo la kutaka kwenda kwa kasi ndipo ufike.

Unapokuwa unaendesha gari, usishawishike kutumia simu yako au kufanya jambo lolote ambalo litakuzuia kuwa makini ukiliendesha gari.

Iwapo utakuwa safarini, usiegeshe gari lako au kuanza kufanya shughuli zako karibu na mto wakati wa mvua.

Ni vyema kusikiliza vituo vya redio na runinga kujifahamisha kuhusu yanayojiri na ni wapi mvua kubwaimenyesha au mafuriko kutokea.

Usitembee kwenye maji au maeneo yenye matope ambayo kuna uwezekano kwamba kuna nyaya za umeme ambazo zimeanguka. Nyumba yako ikifurika maji pia, hakikisha umezima stima.

Iwapo unatembea kwa miguu, tumia fimbo au kijiti kukadiria kina cha maji.

Mafuriko yakitokea eneo ulipo, mara moja kimbilia maeneo yaliyo juu na salama.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *