Mashoga wapo salama

Mashoga wapo salama

Like
887
0
Wednesday, 07 November 2018
Local News

Waziri wa Mambo ya Ndani nchi Kangi Lugola amesema kuwa wapenzi wa jinsia moja hawapo hatarini nchini humo.

Lugola amesema japo ushoga ni kosa la jinai nchini, wanaojihusha na vitendo hivyo hawatishiwi maisha na wala hawaikimbii nchi.

Akizungumza na gazeti la serikali la Habari Leo, Lugola amekanusha kuwa wapenzi wa jinsia moja wapo hatarini.

“Ninachosema ni kuwa Tanzania ni salama na hakuna mtu yeyote anayeweza kusema kuwa sio salama bila ya kuwa na vigezo husika, kama mtu yeyyote anahatarishiwa maisha yake, basi napaswa kwenda polisi na mimi sijapata taarifa zozote kutoka polisi zinazoeleza kuwapo kwa mazingira hatarishi ya watu hao,” Lugola amenukuliwa akisema.

Hata hivyo, wakati Lugola akitoa hakikisho la usalama kwa mashoga, watu 10 wamekamatwa na polisi Zanzibar kwa tuhuma za kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja.

Shirika la kutetea Haki za Binaadamu la Amnesty International limeripoti kuwa wanaume hao 10 wamekamatwa Jumamosi iliyopita katika fukwe ya Pongwe walipokuwa katika harusi ya mashoga. Wengine sita walifanikiwa kuwatoroka polisi.

“Polisi walifika eneo la tukio baada kupewa taarifa na wananchi kuwa kuna harusi ya mashoga inaendelea…Watu hao wanashikiliwa katika kituo cha polisis Chwaka na mpaka sasa hakuna mashtaka yoyote yaliyofunguliwa,” inasema ripoti ya Amnesty.

Sababu hawajakamatwa wakiwa wanafanya ngono, Naibu Mkurugenzi wa Amnesty kwa kanda ya Afrika Mashariki Seif Magongo anahofu kuwa watalazimishwa kufanyiwa vipimo.

Serikali imejitenga na kampeni ya Paul Makonda dhidi ya ushoga

Wiki iliyopita, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda alitangaza kuanza kampeni dhidi ya ushoga kwa kuunda kamati ya watu 17.

Makonda alisema haki za mashoga hazitambuliki kama haki za binaadamu nchini Tanzania na kuzitaka nchi zinazotetea vitendo hivyo kuwachukua mashoga wa Tanzania.

Baada ya kauli hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Tazania ilitoa taarifa kuwa huo si msimamo wa serkali bali mawazo ya Makonda pekee.

Taarifa hiyo ilisema Tanzania itaendelea kuheshimu haki zote za binaadamu kama inavyotakikana na katiba ya nchi pamoja na mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imeisaini na kuiidhinisha.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *