Morsi Azikwa saa chache baada ya kifo

Morsi Azikwa saa chache baada ya kifo

Like
476
0
Tuesday, 18 June 2019
Global News

Rais wa zamani wa Misri, Mohamed Morsi amezikwa saa chache baada ya kufariki dunia akiwa mahakamani siku ya Jumatatu.

Wakili wake ameliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP kiongozi huyo wa zamani alizikwa Mashariki mwa jiji la Cairo asubuhi ya Jumanne familia yake ikiwepo

Morsi,aliyekuwa na miaka 67, alikuwa kizuizini tangu alipoondolewa madarakani mwaka 2013.

Makundi ya watetezi wa haki za binaadamu , ambayo yalikosoa mazingira ambayo Morsi aliwekwa,wametoa wito wa kufanyika uchunguzi kuhusu kifo chake.

Familia yake na wanaharakati wamezungumzia kufo chake na muda ambao aliwekwa katika seli ya peke yake, akizuiwa kutembelewa na wanasheria na familia yake.

Mtoto wake, Abdullah Mohamed Morsi, ameliambia shirika la habari la Uingereza, Reuters siku ya Jumatatu kuwa mamlaka za Misri ziliikatalia familia yake kufanya maziko katika mji yalipo makazi yake.

Kiongozi wa juu wa zamani wa kundi lililopigwa marufuku nchini humo, Muslim Brotherhood, Morsi alikua kiongozi wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia mwaka 2012.

Aliondolewa na kushikiliwa baada ya mapinduzi ya kijeshi mwaka mmoja baadae baada ya kufanyika maandamano makubwa kupinga utawala wake.

Abdul Fattah al-Sisi, Kiongozi wa zamani wa kijeshi, amekuwa madarakani tangu mwaka 2014.

Baada ya kuondolewa madarakani, mamlaka zilipambana na wafuasi wake na wapinzani wengine, na kukamata maelfu ya watu.

Muslima Brotherhood na Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, mshirika wa karibu wa Morsi ni miongoni mwa walioshutumu utawala wa Misri kuhusu kifo cha Morsi.

Kulitokea nini Mahakamani ?

Morsi alikua mjini Cairo siku ya Jumatatu kwa shutuma za kufanya vitendo vya kijasusi ikihusisha kuwa na mawasiliano na kundi la wanamgambo wa kiislamu la kipalestina, Hamas.

Maafisa wanasema aliomba kuzungumza mahakamanu na kuongea kwa dakika tano kutoka kwenye kizimba kilichokua na kioo ambacho alikuwamo ndani yake na washtakiwa wengine.

Dakika chache baadae alizimia wakati wa mapumziko mahakamani hapo.

”Alipelekwa hospitali ambapo alithibitishwa kupoteza maisha,”taarifa ya mwendesha mashtaka ilieleza.

Maafisa wamesema katika ripoti yao kuwa , hakuna majeraha yeyote ambayo yalionekana kwenye mwili wake.

Televisheni ya taifa ilieleza awali kuwa chanzo cha kifo chake ni mshtuko wa moyo.

Mosri tayari alikuwa anatumikia kifungo kutokana na mashtaka matatu yaliyokuwa yakimkabili.Awali alihukumiwa adhabu ya kifo,ambayo baadae ilitenguliwa.

Watu wanazungumza nini baada ya kifo chake ?

”Kifo cha Rais wa zamani, Morsi kimetokea kutokana na kutendewa isivyo haki na serikali, kuwekwa katika gereza la peke yake, alipatiwa huduma mbovu za matibabu, kumzuia kuonana na familia yake na mawakili wake.Alieleza Bi Whitson kwenye taarifa yake.

Shirika la Amnesty International pia limetaka uchunguzi ufanyike kuhusu kifo chake.

Shirika limesema Morsi alikua akiruhusiwa kutembelewa mara tatu tu kwa kipindi cha takribani miaka sita na hakuruhusiwa kuonana na mawakili wake wala daktari.

Mfalme wa Qatar,Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, mshirika mwingine wa Morsi ameeleza masikitiko yake kutokana na kifo chake.

Mbunge wa nchini Uingereza, Crispin Blunt, aliyeongoza jopo la wanasiasa na kutoa tahadhari kuhusu kutendewa kwa Morsi mwaka 2018, ametaka ufanyike ”uchunguzi huru kimataifa”

Tawi la kisiasa la kundi la Muslim Brotherhood, chama cha Freedom and Justice, kimesema kuwa kifo cha Morsi ni ”mauaji”.

Rais wa Uturuki ameshutumu ”wakandamizaji” wa Misri kwa kifo chake na kumuelezea Morsi kuwa shahidi.

Morsi ni nani?

Mohammed Morsi alizaliwa katika kijiji cha El-Awwadh katika jimbo lililopo kwenye delta za mto Nile la Sharqiya mwaka 1951.

Alisomea Uhandisi katika chuo Kikuu cha Cairo katika miaka ya 70 kabla ya kuhamia nchini Marekani ambapo alitunukiwa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Uhandisi.

Morsi aliweka rekodi ya kuwa kiongozi wa kwanza kuchaguliwa katika uchaguzi wa haki na huru mwaka 2012, akiwa kiongozi mwandamizi wa kundi la kiislamu la Muslim Brotherhood ambalo limepigwa marufuku kwa sasa nchini humo.

Hata hivyo utawala wake ulikumbwa na wimbi la maandamano ya wanaharakati ambao walimshutumu yeye na kundi la Muslim Brotherhood kujilimbikizia madaraka.

Baada ya maandamano kuwa makubwa, na wafuasi wa Morsi kushambulia wapinzani wake, jeshi likiwa chini ya rais wa sasa Abdel Fattah el-Sisi liliendesha mapinduzi na kumng’oa Morsi madarakani, Juni 2013.

Jeshi liliendelea kupambana na wafuasi wa Morsi baada ya mapinduzi, na zaidi ya wafuasi wake 1,000 waliuawa Agosti 2013.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *