Mwanaharakati wa Rwanda awa mmoja kati ya wanawake 10 mashuhuri duniani

Mwanaharakati wa Rwanda awa mmoja kati ya wanawake 10 mashuhuri duniani

Like
629
0
Thursday, 12 April 2018
Global News

Wanawake hao wanajifunza kukubali yaliyawatokea wakati wa vita vya kimbari

Mwanaharakati wa maswala ya wanawake nchini Rwanda Godelive Mukasarasi amewekwa kwenye orodha ya wanawake 10 mashuhuri duniani.
Tuzo aliyopewa na Marekani Bi Godelive Mukasarasi inatokana na juhudi za shirika aliloanzisha nchini Rwanda la SEVOTA kusaidia wakinamama walionusurika na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.
Amewekwa kwenye orodha hiyo na nchi ya Marekani ambao hivi karibuni walitunukiwa tuzo ijulikanayo kwa jina”International women of Courage ” kutokana na shughuli za shirika lake la SEVOTA ambalo husaidia wanawake waliobakwa wakati wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda pamoja na watoto waliozaliwa kutokana na kitendo hicho.
Shirika hilo limekuwa likisaidia wakinamama hao kujijenga kimaisha, kupokea yaliyowapata na kuwapa upendo watoto waliozaa kwa namna hiyo.

Shirika hilo aliloanzisha limeweza kukusanya watu wasiopungua elfu 10 ambao ni wanawake wajane wa mauaji ya kimbari na watoto yatima.
Kadhalika tuzo aliyopewa ni baada ya kile kilichotajwa kuwa juhudi zake kupigania kosa la ubakaji kuwa miongoni mwa makosa ya uhalifu wa kivita.

“Ni kweli kwamba mwaka 96 Rwanda ilipotunga sheria ya kuadhibu waliofanya mauaji ya kimbari,tulipaaza sauti wanaharakati wote wa akinamama pia kwa msaada wa wabunge wanawake wote walisimama kwa kauli moja kwamba waliofanya makosa ya ubakaji lazima wawekwe katika ngazi ya kwanza ya wauwaji wanaohukumiwa adhabu kali” alieleza Mukasarasi
Wakinamama hao husaidiwa kujikimu kimaisha wakifanya kazi katika mashirika mbali mbali, lakini kubwa zaidi ni ushauri nasaha wa jinsi ya kukabiliana na matatizo yaliyowapata wakati wa mauaji ya kimbari na kuwaonesha upendo watoto wao waliozaa wakati wa kubakwa.

 

 

Comments are closed.