sakata la kutekwa kwa mo dewji giza nene

sakata la kutekwa kwa mo dewji giza nene

Like
653
0
Thursday, 18 October 2018
Local News

Tukio la kutekwa bilionea Mohammed Dewji, 43, Alhamisi ya wiki iliyopita bado limesalia kuwa ni fumbo lisilokuwa na jibu.

Mpaka kufikia leo bado haijulikani ni akina nani waliomteka na wapi walipomficha na lipi hasa kusudio la kumteka mfanya biashara huyo maarufu kama Mo.

Mo alikwapuliwa na watu wasiojulikana nje ya hoteli moja jijini Dar es Salaam alipokuwa akienda kufanya mazoezi. Toka hapo, giza nene limetanda juu ya tukio hilo, licha ya hatua kadhaa ambazo mamlaka za nchi na familia imezichukua.

Toka siku ya kwanza ya tukio polisi kupitia Kamanda wa Dar es Salaam wamekuwa wakiuhakikishia umma kuwa ulinzi umeimarishwa na uchunguzi unafanyika kwa kasi na weledi. Maeneo yote ya kutoka na kuingia jiji la Dar es Salaam ikiwemo fukwe za bahari zinakaguliwa.

Hatahivyo, si wote wanaoonekana kuridhishwa na kasi ya uchunguzi. Mathalan, suala la picha za kamera za CCTV zilizonasa tukio hilo ni kizungumkuti. Polisi wanasema kamera za hoteli hazikunasa tukio hilo ipasavyo na kuwapa ugumu wa kung’amua undani wa tukio hilo.

Hata hivyo, waziri kivuli wa mambo ya ndani na mbunge wa upinzani Godbless Lema ameonesha wasiwasi wake juu ya kauli za mamlaka akitaka picha hizo ziwekwe wazi ili wananchi wasaidie katika utambuzi wa watekaji na magari yaliyotumika.

Gazeti la Mwananchi la jana Jumatano Oktoba 17 pia limeandika kuwa licha ya uwepo wa kamera za CCTV hotelini hapo, majengo mengi yanayoizunguka hoteli hiyo na barabara ambayo yadaiwa kutumiwa na watekaji imesheheni kamera za CCTV.

Upinzani na watumiaji wa mitandao Tanzania pia wamekuwa wakiomba serikali ikaribishe mashirika ya upelelzi ya nje kama FBI na Scotland Yard kuja kusaidia kutatua fumbo hilo lakini serikali kupitia waziri wa mambo ya ndani Kangi Lugola na naibu wake Hamad Masauni wote kwa nyakati tofauti wametupilia mbali ombi hilo wakisema vyombo vya ndani vya ulinzi vinauwezo wa kutosha.

Jumla ya watu 26 walikamatwa kutokana na tukio hilo na mpaka jana Jumanne 19 waliachiwa kwa dhamana.

Baada ya kukaa kimya kwa siku nne, familia ya Mo ilijitokeza siku ya Jumatatu na kutangaza kuwa watatoa zawadi ya Shilingi za kitanzania bilioni moja kwa yeyote atakayewapatia taarifa zitakazofanikisha kupatikana kwa Mo.

Msemaji wa familia hiyo, Azim Dewji amesema familia inapitiakipindi kigumu na wanashukuru kwa dua na faraja wanayopewa na Watanzania.

Licha ya kutangazwa kwa dau hilo siku tatu zilizopita, bado mpaka sasa hajapatikana.

Mo anakisiwa kuwa na utajiri wa $1.5 bilioni kwa mujibu wa jarida la masuala ya fedha la Forbes na kumfanya kuwa tajiri namba moja Afrika Mashariki na bilionea mwenye umri mdogo zaidi Afrika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *